Ruto ateleza akijisifu ameibadilisha Kenya
KATIKA mahojiano na runinga ya Al Jazeera Novemba 9, 2025, Rais William Ruto alisifu hatua za serikali yake, akidai kuwa uchumi, kilimo, elimu, na usajili wa bima ya afya ya jamii zimeimarika kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wake.
Ruto alisisitiza kuwa juhudi zake zimefanya Kenya kupata mafanikio makubwa. “Nimerekebisha uchumi. Kenya sasa imeorodheshwa kama ya sita kwa ukubwa wa uchumi barani Afrika kutokana na hatua nilizochukua.”
Ukaguzi wa takwimu rasmi unaonyesha kuwa madai haya kuhusu uchumi yana ukweli. Kulingana na ripoti ya Hali ya Uchumi Ulimwenguni ya IMF ya Aprili 2025, Kenya ilikuwa uchumi wa sita kwa ukubwa barani Afrika, ikishuka kutoka nafasi ya nane mwaka 2022. Hii inaashiria ukuaji wa uchumi wa nchi, lakini ni muhimu kuzingatia kuwa ukuaji huu unachangiwa na ukuaji wa bara kwa jumla na si tu mafanikio binafsi ya serikali.
Nchi zilizokuwa mbele yake ni Afrika Kusini, Misri, Algeria, Nigeria na Morocco.
Ruto pia alijisifu kuhusu soko la hisa la Nairobi, akidai: “Soko letu la hisa limechaguliwa kuwa soko bora la hisa barani Afrika.” Hata hivyo, hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai haya.
Uchambuzi wa Morgan Stanley Capital International (MSCI) unaonyesha kuwa NSE ilikuwa ya tatu kwa faida kwa dola barani Afrika kufikia Septemba 2025 nyuma ya Morocco na Nigeria. Hivyo, madai haya hayana msingi wa ukweli, ingawa sekta ya hisa inaonyesha ukuaji wa uwekezaji.
Katika kilimo, Rais Ruto alidai: “Tumekebisha kilimo. Leo tumeongeza uzalishaji wa mahindi kwa asilimia 50 kutoka magunia 44 milioni kila mwaka hadi karibu magunia 70 milioni mwaka uliopita.”
Kwa mujibu wa ripoti ya Uzalishaji wa Kilimo Kitaifa National 2025, uzalishaji wa mahindi mwaka 2024 ulikuwa magunia 44,759,111 ya kilo 90, na makadirio ya magunia 70 milioni 2025 bado hayajathibitishwa. Hivyo, madai yake hayawezi kuthibitishwa kikamilifu, kwani yanategemea makadirio na si uzalishaji halisi.
Ruto aliongeza: “Tumesharekebisha mfumo wa elimu. Nimeajiri walimu 100,000 zaidi, kujenga madarasa 23,000, na kuanzisha mfumo mpya wa ufadhili wa wanafunzi ambao sasa umefanya vyuo vyetu vyote kuwa endelevu.”
Hata hivyo, takwimu za Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) zinaonyesha kuwa walimu walioajiriwa ni 76,000, ikijumuisha walimu wa kudumu na wa vibarua.
Mpango wa kuajiri walimu 24,000 unaendelea na bado haujakamilika, huku takwimu za madarasa aliyodai kujenga zikikosa kubainika. Mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo uliozinduliwa mwaka 2023 ulisimamishwa na korti mwaka 2024, lakini utekelezaji wake ulibadilishwa Machi 2025. Kwa hivyo, madai haya hayathibitishwi kikamilifu.
Madai kuhusu usajili wa bima ya afya ya jamii yanaonekana kuwa sahihi.
Ruto alisema: “Tulikuwa na watu milioni 8 kwenye bima ya afya ya jamii. Leo tuna watu 27.2 milioni.” Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Aden Duale, idadi ya Wakenya waliosajiliwa sasa ni zaidi ya 27 milioni, ikithibitisha mafanikio katika sekta hii muhimu ya kijamii.
Ukaguzi wa madai yote ya Rais Ruto unaonyesha mchanganyiko wa ukweli na makadirio. Uchumi na usajili wa bima ya afya zimeimarika, lakini madai kuhusu soko la hisa, kilimo na elimu hayajathibitishwa kikamilifu.
Hii inaonyesha kwamba ingawa serikali inafanya maendeleo katika baadhi ya sekta, baadhi ya madai ya Ruto yanahitaji tahadhari na ukaguzi zaidi.
Wachanganuzi wa siasa na uchumi wanasema Rais Ruto ameonyesha juhudi za kuimarisha sekta tofauti, lakini ukweli unaonyesha kwamba baadhi ya madai yake yameongezwa chumvi.