Habari

“Ruto tumemalizana, hatutarudi kwa utumwa wako 2027” – Gachagua

Na MWANGI MUIRURI December 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumapili alimwaambia Rais William Ruto asahau kura za Mlima Kenya mnamo 2027 kwa kuwa wakazi wa eneo hilo huwa hawavumilii  usaliti wa kisiasa.

Bw Gachagua amesema eneo hilo litasaka ushirikiano na viongozi wengine mnamo 2027 lakini si Rais Ruto tena. Alimtaja kinara wa upinzani Raila Odinga,  mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kama viongozi ambao watashirikiana nao ifikapo 2027.

“Kura za Mlima Kenya hazitawahi kumwendea mtu yeyote kwa njia rahisi. Ije mvua au jua, kura zetu hazitawahi kutupeleka katika utumwa. Kivyovyote vile 2027 kura za Mlima Kenya hazitamwendea Rais Ruto, “akasema Bw Gachagua wakati wa mahojiano na runinga ya Inooro.

“Aidha wale ambao wanatoka Mlima Kenya na bado wako kwa mrengo wa Rais Ruto watatengwa na hawatashinda kiti chochote,” akaongeza.

Gachagua wakati wa mahojiano katika yaliyokuwa makazi yake rasmi akiwa Naibu Rais, mtaani Karen mjini Nairobi mnamo Desemba 1, 2024. PICHA | EVANS HABIL

Rais Ruto alishinda kura za 2022 huku Bw Gachagua akichukua nafasi ya naibu rais. Hata hivyo, uhusiano kati ya wawili hao umedorora kwa miaka miwili kiasi kuwa Bw Gachagua alingólewa kwenye wadhifa wake.

“Jamii ambayo inataka kushirikiana na sisi mnamo 2027 ni nyingi. Rais Ruto anaendelea kutengwa kwetu,”

Rais Ruto aliamrisha wandani wake wamng’oe Bw Gachagua na kuchangia kuondolewa kwake afisini mnamo Oktoba 17. Profesa Kithure Kindiki aliapishwa kama naibu rais mnamo Novemba 1 na akachukua nafasi ya Bw Gachagua.

Bw Gachagua  anaonekana kunufaika na wimbi la maasi dhidi ya utawala wa Rais Ruto kwenye ukanda wa Mlima Kenya hasa baada ya kuondolewa kwenye wadhifa wake.

“Sisi katika eneo hili hatusamehi usaliti na tunaichukulia kama dhambi isiyosamehewa,” akasema.

Wiki jana, Rais Ruto alikutana na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ambao walikuwa na uhasama mkali naye kuelekea uchaguzi wa 2022. Bw Kenyatta alimuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi huo.

Rais William Ruto (kulia) alipomtembelea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta nyumbani kwake Gatundu, Kiambu, mwezi huu. PICHA | PCS

Jumapili, Bw Gachagua alipuuza mazungumzo kati ya Rais Ruto na Bw Kenyatta  akisema yalikuwa ya masuala ya kibinafsi wala hayana athari zozote kuhusu msimamo ambao umechukuliwa na wakazi wa Mlima Kenya.

“Hata Uhuru kama kiongozi wetu anajua kuwa wakazi wa Mlima Kenya hawachukui amri kutoka kwa mtu yeyote. Mlima Kenya hutana haja na Ruto tena wala hatutatishwa, kuhukumiwa au kuhadaiwa naye tena,” Bw Gachagua.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira aliendelea kuelekeza mashambulizi makali akisema kuwa kwa sasa wanatafuta njia ya kujiresha katika uongozi wa nchi.

“Tulikuonya dhidi ya kutusaliti lakini hakutusikiza. Umechimba shimo Mlima Kenya na sasa lazima uishi kwenye shimo hilo kwa sababu sasa hatukutaki eneo hili,” akasema.

Kwa wale ambao bado wapo serikalini na wanaunga mkono utawala wa sasa wakiwa wanatoka Mlima Kenya, alisema kisingizio chao kuwa wanafanya hivyo ili kupata maendeleo ni hadaa tupu.

Gachagua ataka IEBC ibuniwe haraka

Wakati huo huo, kiongozi huyo alitoa wito wa kuharakishwa kwa mchakato wa kubuni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) akisema kuwa kuna viongozi ambao wanamsubiri abuni chama kipya ili wajiuzulu na kuwania viti kwa mara nyingine.

“Hata kuna Wakenya ambao wangetaka kuwatimua wabunge wao ili wawachague wale ambao si wasaliti na wanawasikiza,” akasema.

Alipuuza madai kuwa wakazi wa Mlima Kenya wamekuwa na tabia ya kueneza ukabila, akisema hiyo ni njama ambayo imepangwa kwa sasa na utawala wa Kenya Kwanza kutenga eneo hilo.