Seneti yapendekeza kamati ya wanachama 11 kuchunguza hoja ya kutimuliwa Waiguru
Na CHARLES WASONGA
BUNGE la Seneti limependekeza kubuniwe kamati maalum ya wanachama 11 kuchunguza madai ya madiwani waliopitisha hoja ya kumtimua Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru.
Lakini licha ya pendekezo hilo la Kamati ya Kuratibu Shughuli za Seneti (SHBC), kiranja wa wengi Seneta Irungu Kang’ata amesema Ijumaa kuwa pendekezo hilo litawasilishwa kwa kikao cha maseneta Jumanne ili ama liidhinishwe au likataliwe.
“Kikao cha maseneta wote kitaamua Jumanne ikiwa suala hili litashughulikiwa kupitia kamati maalum au kikae na kupendekeza gavana mwenyewe aagizwe kujiwasilisha ukumbini ajitetee kuhusu mashtaka dhidi yake,” Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a amewaambia wanahabari baada ya mkutano huo wa SHBC ulioongozwa na Spika Kenneth Lusaka.
Licha ya Bw Kang’ata kudinda kufichua majina ya wanachama waliopedekezwa kuketi katika kamati hiyo maalum, Taifa Leo imepata orodha ya majina hayo kutoka kwa seneta mmoja ambaye aliomba jina lake libanwe.
Kutoka upande wa Jubilee waliopendekezwa ni; Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Mohamed Muhammud (Mandera) Abshiro Halakhe (Seneta Maalum), Gideon Moi (Baringo), Anuari Oloitiptip (Lamu) na Beth Mugo (Seneta Maalum).
Upande wa Nasa waliopendekezwa ni pamoja na; Cleophas Malala (Kakamega), Beatrice Kwamboka (Seneta Maalum), Judith Pareno (Seneta Maalum), Moses Kajwang’ (Homa Bay) na Enock Wambua (Kitui).
Gavana Waiguru aliona kivumbi Jumanne baada ya madiwani 23 kati ya 33 kupitisha hoja ya kumwondoa ofisini kwa tuhuma za ufisadi, ubadhirifu wa pesa za umma na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake.
Jaribio la Bi Waiguru kuitaka mahakama kubatilisha uamuzi huo ulikataliwa na Jaji wa Mahakama Kuu Weldon Korir. Madai ya Gavana huyo kwamba hoja hiyo ilijadiliwa na kupigiwa kura kinyume cha agizo la mahakama la kuisimamisha, ilikataliwa na Jaji Korir aliyeshikilia kuwa bunge hilo halikukaidi agizo lolote.