Serikali yaahidi kukomesha ugaidi unaovuruga elimu Wajir
Na WANDERI KAMAU
SERIKALI Jumatano ilisema imebuni mpango ambao utahakikisha kwamba shughuli za masomo hazitaathiriwa katika Kaunti ya Wajir.
Hii ni kufuatia rai za walimu wanaofunza katika kaunti hiyo kutaka kuhamishwa kutokana na mashambulio ya mara kwa mara kutoka wanamgambo wa kundi la Al Shabaab.
Wiki iliyopita, walimu watatu ambao si wenyeji waliuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la Al Shabaab.
Lakini Jumatano, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisema kuwa wizara yake inashauriana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba shughuli za masomo haziathiriwi.
Kwenye ziara katika kaunti hiyo, Dkt Matiang’i alilalama kwamba vitisho kutoka kwa makundi hayo ndivyo vimekuwa vikiwatia wasiwasi walimu.
“Tumejitolea kikamilifu kulikabili janga hili ili kuhakikisha haliwanyimi haki watoto kupata elimu,” akasema.
Kauli yake inajiri baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kutangaza kuwahamisha karibu walimu 200 kutoka kaunti hiyo.
Kulingana naye, mpango huo utahakikisha kwamba kando na kupewa ulinzi wa kutosha, wanapewa malipo maalum.
Maeneo yaliyoathiriwa sana na Wajir Mashariki, Wajir Magharibi, Eldas na Tarbaj.
Jumanne, mamia ya walimu wanaohudumu katika eneo hilo walifika katika afisi za tume hiyo jijini Nairobi, wakitaka kuhamishwa, wakidai kuhangaishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa eneo hilo.
Uhai ni muhimu
“Hatuwezi kuendelea kufunza katika mazingira ambayo hatutakiwi. Uhali wetu ni muhimu, hivyo lazima asasi husika ziwajibike ifaavyo,” akasema mwalimu mmoja.
Shambulio hilo, ambalo lilifanyika mwendo wa saa saba usiku pia lilipelekea mwalimu mwingine kupata majeraha mabaya ya risasi.
Wakuu mbalimbali wa vyama vya walimu wamejitokeza kutetea rai zao, kwa msingi kwamba hawawezi kuendelea kuuawa bila ya vikosi vya usalama kuwajibika.“Imefikia kiwango ambacho lazima maslahi ya walimu yashughulikiwe.”
Kufikia Jumatatu, zaidi ya shule kumi zilikuwa zimefungwa katika eneo hilo, walimu wakilalama kwamba hawangeendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo si salama.
Hilo lilipelekea viongozi kutoka eneo hilo kutishia kufanya maandamano katika afisi za TSC, kupinga kuhamishwa kwa wao.
Wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale, viongozi hao walisema kuwa tume hiyo inalibagua eneo hilo bila sababu zozote.
“Tatizo la ugaidi linatokana na ulegevu wa asasi za usalama. Tusiwadhulumu watoto wetu kwa kutowajibika kwa taasisi hizo,” akasema Bw Duale.