Jamvi La Siasa

Sumu iliyoua Nasa yarudi kumaliza Azimio

Na BENSON MATHEKA July 20th, 2024 3 min read

SUMU iliyoua miungano ya Nasa na Cord sasa inaonekana kusambaratisha Muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Kuna dalili za wazi kuwa muungano huo ulioundwa kabla ya uchaguzi wa Agosti 2022 kushindana na Rais William Ruto, unavunjika, huku vinara wenza wakiwa na misimamo tofautia kisiasa.

Kiini cha migawanyiko mikali ya hivi majuzi kati ya vinara wenza wa muungano huo ni mzozo kuhusu iwapo unafaa kuwa sehemu ya serikali ya Rais William Ruto.

Kilichoanza kama ODM kuunga mkono wito wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa na serikali ya umoja wa kitaifa, sasa kimebadilika na kuwa mgawanyiko mkubwa.

Huku chama cha Raila Odinga cha ODM kikimezea mate kujiunga na serikali, vyama tanzu vingine vya muungano vinapinga wazo hilo.

Wiper cha Bw Kalonzo Musyoka, DAP- K cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na Narc Kenya cha Martha Karua na Jubilee – baadhi ya vyama vikuu katika muungano wa vyama 23 – vimepinga wazo hilo.

Lakini matukio mabaya ya Jumatano ambapo viongozi walishambuliwa na wahuni yanaweza kuwa msumari wa mwisho katika jeneza la Azimio.

“Hatutakuwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa au serikali nyingine yoyote na Kenya Kwanza,” Bw Musyoka alisema akisoma taarifa ya Azimio Jumatano kabla ya kuvamiwa na wahuni.

Kujiunga au kutojiunga na serikali kunaonekana kuwa sumu ya kuua Azimio huku vyama tanzu vikishinikiza kongamano la kitaifa na sio mazungumzo na vile vile mageuzi makubwa katika serikali na haki kwa waasiriwa wa maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali.

Tofauti za vinara wenza na ODM ni mbaya sana hivi kwamba taarifa ya muungano huo, iliyokuwa ikisomwa na Bw Musyoka Jumatano, ilikatizwa baada ya wahuni kuvamia na kufukuza wanahabari katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (Joof) jijini Nairobi.

Taarifa ya azimio iliyosomwa na makamu huyo wa rais wa zamani ilitofautiana na taarifa ya awali kutoka kwa mkutano wa kundi la wabunge wa ODM.

Ishara kwamba ODM haikukubaliana na washirika wake katika Azimio ilionekana Bw Odinga alipoondoka ukumbini kabla Bw Musyoka kusoma taarifa akiwa na kiongozi wa Party of National Unity Peter Munya, Seneta wa Kitui Enoch Wambua, na viongozi wengine wachache.

Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior asema hatua ya Raila kuondoka ilitokana na muungano huo kutokubaliana kuhusu mazungumzo ya kitaifa na kujiunga na serikali.

“Tumekuwa tukitofautiana hapo awali lakini haijawahi kufikia viwango vilivyoonekana Jumatano. Ni utovu wa kutovumilia,” akasema Bw Kilonzo Junior.

“Ninavyofahamu, pia ni ishara kwamba washirika wetu katika Azimio pia wamechoshwa na Kalonzo. Sioni Azimio ikiwepo. Niamini,” aliongeza.

Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema kila mara wamekuwa wakishinikiza kuwepo kwa kongamano la kitaifa ambapo kila mtu ana nafasi ya kushiriki na wala sio suluhu ya dharura.

Akizungumza katika mahojiano na runinga moja nchini, diwani wa Kileleshwa Robert Alai alisema anaamini Azimio imetimiza lengo lake na sasa inapaswa kuvunjwa.

“Tunaona hali ambayo tunaongozwa na watu ambao wana masilahi tofauti, tulipaswa kushinda uchaguzi na hivyo ikiwa huu utakuwa mwisho wa Azimio, na iwe hivyo,’ aliongeza.

Nyufa katika muungano huo zilianza kujitokeza Februari mwaka jana maswali yalipoanza kuulizwa iwapo kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi bado alikuwa sehemu ya muungano huo.

Seneta huyo wa zamani wa Baringo hakushiriki katika shughuli zozote za muungano huo huku ukimya wake ukisababisha Seneta Maanzo kusema ni Wiper na ODM pekee ambavyo vilibaki katika kwenye muungano huo baada ya wabunge wengi wa Jubilee kushirikiana na muungano wa Rais Ruto wa Kenya Kwanza.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, Azimio inafuata watangulizi wake ikiwa ni pamoja na muungano wa NASA na Cord.

Cord iliyoanzishwa mwaka wa 2012 kabla ya uchaguzi wa 2013 ilijumuisha angalau vyama 12 huku Bw Odinga akiwa kiongozi wake, Bw Musyoka, alikuwa mgombea mwenza na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na chama chake cha Ford-Kenya wakiwa vinara wakuu.

Vyama vingine vilikuwa Kenya Social Congress, Kadu-Asili, Peoples Democratic Party, Chama Cha Mzalendo, Muungano Party, Federal Party of Kenya, United Democratic Movement, Chama Cha Mwananchi na Mkenya Solidarity Movement.

Muungano huo haukudumu kuona uchaguzi wa 2017 na ulivunjwa baada ya miaka mingi ya kutofautiana na kuzozana kisha NASA ikaundwa.

Muungano huo uliundwa na watu waliofahamiana baada ya kushawishi Musalia Mudavadi, ambaye aliwania urais 2013 lakini sasa akaacha azma yake ya urais na kuunga Bw Odinga.

NASA ulipasuka baada ya kuapishwa kwa Bw Odinga katika bustani ya Uhuru. Tofauti ziliongezeka baada ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzika tofauti zake na Bw Kenyatta Machi 2018.

Aidha, Bw Odinga alikataa kuidhinisha mmoja wa vinara wenza katika Nasa akidai walikosa kujitokeza wakati wa kujiapishwa kwake.

Sawa na Cord, Nasa ilikabiliwa na hali ya kutoaminiana, usaliti na ushindani uliopelekea muungano huo kufa.