TUNARUDI TENA CHAMA KIMOJA? Demokrasia hatarini
Na BENSON MATHEKA
Kenya inarejea taratibu katika utawala wa chama kimoja kufuatia matukio ya hivi majuzi ya wanasiasa kujiunga na Serikali.
Dalili zaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ijayo, kuna hatari ya kurudisha nyuma maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi ambayo Wakenya wamekuwa wakifurahia kwa miaka 26 iliyopita.
Tangu Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga asalimiane na Rais Uhuru Kenyatta, wanasiasa wa upinzani wamefuata nyayo na kukubali kuunga serikali ya Jubilee.
Siku mbili kabla ya muafaka wa Rais Kenyatta na Raila, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ni mwandani wa Rais, alibashiri kuwa Kenya itakuwa chini ya utawala wa chama kimoja kabla ya mwisho wa mwaka huu.
“Kufikia Desemba 2018, Kenya itakuwa demokrasia ya chama kimoja,” aliandika Bw Kuria kwenye ukurasa wake wa Facebook bila kufafanua.
Hali hiyo inaendelea kujitokeza na kufikia wakati huo, vyama vikubwa vya kisiasa vitakuwa kwa jina tu bila uwezo wa kukosoa serikali kama ilivyo katika nchi za Rwanda na Uganda.
Japo viongozi wa vyama hivyo wanasisitiza wangali katika upinzani na wanachounga ni vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo pekee, dalili ni wazi kuwa wanaelekea serikalini.
Raila mwenyewe amekoma kukosoa serikali na amenukuliwa akisema ni kwa sababu anawasiliana moja kwa moja na Rais Kenyatta. Wabunge wa chama chake cha ODM wamechukua misimamo ndani ya chama cha Jubilee, baadhi wakimuunga Rais Kenyatta na wengine wakimuunga Naibu Rais William Ruto.
Chama cha Wiper ambacho pamoja na ODM, Ford Kenya na Amani National Congress vinaunda muungano wa upinzani wa NASA, pia kimetangaza kushirikiana na serikali na kuna fununu kwamba huenda kiongozi wake Kalonzo Musyoka akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini.
Baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula alijitangaza kuwa kiongozi rasmi wa upinzani, hatua ambayo wadadisi wanasema ni kejeli.
“Wetangula amekaribia serikali kama vinara wenzake katika NASA. Tofauti yake na Bw Odinga na Bw Musyoka ni kuwa, anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika chama cha Jubilee,” alisema mbunge mmoja kutoka Rift Valley ambaye hakutaka kutajwa jina.
Siku tatu baada ya Wiper kutangaza kuwa kitashirikiana na serikali, Bw Musyoka alimwalika Bw Wetangula katika kilichotajwa kama juhudi za kumshawishi kufuata nyayo za vinara wenzake.
Duru zinasema kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi huenda akapatiwa wadhifa mkubwa serikalini hatua ambayo huenda ikamvuta Wetangula upande wake iwapo juhudi za kuunganisha vyama vyao zitafaulu.
Bw Mudavadi amekubali kuunga vita dhidi ya ufisadi na Ajenda Nne za Maendeleo za Serikali ya Jubilee na iwapo atapatiwa wadhifa serikali hataweza kukosoa serikali.
Kulingana na Profesa David Monda wa City University, New York kurejea kwa utawala wa chama kimoja kwa hali yoyote ni hatari.
“Ni suluhu mbadala na hatari kwa tofauti za kisiasa Kenya,” asema.