Michezo

Uhispania wafinya Italia, Ureno na Ubelgiji kazi ipo

June 22nd, 2024 2 min read

GELSENKIRCHEN, UJERUMANI

KOCHA Luis de la Fuente amemiminia sifa vijana wake wa Uhispania baada ya kufanya mabingwa watetezi Italia waonekana kawaida kwa kuwafinya 1-0 na kutinga 16-bora kwenye Kombe la Ulaya (Euro) hapo Alhamisi.

Mabingwa wa Euro 1964, 2008 na 2012, Uhispania walizamisha Waitaliano kupitia bao la kujifunga kutoka kwa beki Riccardo Calafiori dakika ya 55.

Lamine Yamal, ambaye babake anatoka Morocco na mama anatoka Equatorial Guinea, na Nico Williams aliye na asili ya Ghana, walikuwa mafundi katika kuangushwa kwa Italia baada ya kusumbua vilivyo katika wingi ya kulia na kushoto, mtawalia.

Krosi ya Williams kwa nahodha Alvaro Morata ilizalisha bao la ushindi baada ya Calafiori kujifunga akijaribu kuondosha hatari.

Italia, ambao wamekutana na Uhispania mara tano katika Euro tangu mwaka 2008, watashukuru kipa Gianluigi Donnarumma kwa kufungwa bao moja pekee.

Donnarumma alipangua makombora mengi tu hatari katika ushindi huo wa kihistoria kwani Uhispania ilishinda Italia mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza kabisa. Ilishinda Italia 2-1 mwaka 2021 na 2-1 mwaka 2023 kwenye Ligi ya Mataifa ya Ulaya (Uefa Nations League).

Ulikuwa ushindi mtamu dhidi ya Italia ambao hawakuwa wamepoteza michuano 10 mfululizo kwenye Euro.

Hapo Alhamisi, Uhispania walikuwa wamepewa na kompyuta maalum ya Opta asilimia 45.1 ya kulaza Italia, 27.0 kutoka sare na 27.9 kupoteza.

Uhispania hawakusikitisha kwani walidhibiti kila idara na kuvuna ushindi huo muhimu baada ya kutuma makombora 20 dhidi ya nne, kumiliki mpira kwa asilimia 58 dhidi ya 42, kusuka pasi 590-440 na kupata kona tano dhidi ya mbili.

“Nafurahia na kujivunia jinsi walizima mabingwa watetezi. Wataimarisha viwango vyao katika mechi zijazo. Hakuna timu bora kuliko yetu…Hatutajisahau kwa sababu ya ushindi huu,” akasema Fuente.

Kabla makala haya ya 17 kuanza Juni 14, Opta iliipa Uingereza asilimia kubwa ya kutwaa taji ikiwa na asilimia 19.9 na kufuatiwa na Ufaransa (19.1), Ujerumani (12.4), Uhispania (9.6), Ureno (9.2), Uholanzi (5.1), Italia (5.0), Ubelgiji (4.7), Denmark (2.2) na Croatia (2.0).

Kocha wa Italia, Luciano Spalletti anajilaumu kwa kipigo hicho. “Labda ningewapa wachezaji mapumziko zaidi kwa sababu walipumzika siku moja na nusu pekee.

Kulikuwa na pengo kubwa kati ya timu hizi. Kila mara tulisukumwa kabisa na hatukuweza kuziba mianya,” akasema Spalletti ambaye vijana wake lazima wapige Croatia hapo Jumatatu ili kujihakikishia tiketi ya 16-bora.

Ureno, Ubelgiji zina kibarua kigumu leo

Leo itakuwa zamu ya mabingwa wa mwaka 2016 Ureno na Uturuki ambao nafasi nzuri kwenye Euro ni nusu-fainali mwaka 2008.

Timu hizi zinakutana kwa mara ya nne katika Euro, huku Ureno ikijivunia kutwaa ushindi mara tatu mfululizo kwa jumla ya mabao 5-0.

Wareno pia walilaza Uturuki 3-1 walipokutana mara ya mwisho katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022.

Mshindi kati ya Ureno na Uturuki ataingia moja kwa moja raundi ya 16-bora.

Mechi nyingine inayotarajiwa kuwa moto ni kati ya Ubelgiji na Romania.

Wabelgiji walianza kampeni kwa kupoteza 1-0 mikononi mwa Slovakia kwa hivyo hawana jingine ila kushinda la sivyo wajipate pabaya zaidi.

Romania wamejaa motisha ya kutwanga Ukraine 3-0 katika mechi yao ya kwanza.

Ubelgiji na Romania zinakutana mashindanoni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1993.

Mara ya mwisho walikutana ilikuwa katika mchuano wa kirafiki wakati Romania walitamba 2-1 mwaka 2012.

MATOKEO YA ALHAMISI:

Kundi C – Slovenia 1-1 Serbia, Denmark 1-1 Uingereza

Kundi B – Uhispania 1-0 Italia

RATIBA YA LEO:

Kundi F: Georgia vs Czechia (4.00pm), Uturuki vs Ureno (7.00pm)

Kundi E – Ubelgiji vs Romania (10.00pm)

RATIBA YA KESHO:

Kundi A – Uswisi vs Ujerumani (10.00pm), Scotland vs Hungary (10.00pm)