Habari

Uhuru aangusha bakora

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

CHARLES WASONGA na IBRAHIM ORUKO

MISUKOSUKO ya kisiasa ambayo imekuwa ikitokota katika chama tawala cha Jubilee hatimaye ililipuka Jumatatu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kufanya mageuzi makubwa katika uongozi wa chama hicho katika Seneti.

Rais aliwafurusha wandani wa naibu wake William Ruto na mahali pao kuwaweka washirika wake.

Seneta wa Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio aliteuliwa kiongozi wa Wengi Seneti, nafasi ambayo imekuwa ikishikiliwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata alipandishwa hadhi na kupewa wadhifa wa kiranja wa wengi ambao umekuwa ukishikiliwa na Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika.

Naibu wake atakuwa Seneta Maalum, Bi Farhiya Ali Haji.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya mabadiliko hayo kutangazwa na Ikulu, Bw Murkomen na Bi Kihika waliandaa mkutano na wanahabari na kutangaza kuwa hawatang’atuka afisini kwa kuwa mkutano uliowabandua kwa nyadhifa hizo, haukupangwa inavyostahili na pia kukosa idadi ya maseneta kuendesha shughuli hiyo.

“Ikulu ya Rais si makao makuu ya chama cha Jubilee na kwa hivyo tutapuuza tangazo la kuondolewa kwetu,” alisema Murkomen, akiongeza kuwa kuondolewa kwao hakuna mashiko na kanuni muhimu za Bunge hazikuzingatiwa.

Wawili hao walipuuza dai la Ikulu kuwa maseneta 20 walihudhuria mkutano huo na badala yake kutoa orodha yao wenyewe inayoonyesha maseneta 22 wanaoegemea kwa Bw Ruto hawakuhudhuria mkutano huo.

Walitangaza kuwa hawataondoka kwa afisi zao na kufichua kuwa wamemwandikia Spika Ken Lusaka wakitaja udhaifu wa kisheria uliopo katika hatua ya Rais na watu wake.

Wakati huo huo, wandani wa Bw Ruto walitishia kupinga hatua hiyo mahakamani.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Bw Caleb Kositany alisema kuondolewa kwa Bw Murkomen na Bi Kihika kutoka nyadhifa hizo ni batili na kinyume cha Katiba ya Jubilee.

“Wale waliotekeleza mabadiliko hayo walishiriki mchakato haramu na usiokubalika na Katiba yetu. Na bila shaka tutaenda mahakamani kubatilisha mageuzi hayo kwa sababu hayakuidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama chetu,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa simu Jumatatu.

Bw Kositany akaongeza: “Kiongozi wa Chama hafai kuhusishwa katika shughuli kama hizi zinazovunja sheria. Mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi haukuwa halali na hivyo ulifanya mageuzi haramu.”

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alisema, kuanzia sasa hawatakubali mikutano ya Kundi la Wabunge (PG) wa Jubilee kufanyika katika Ikulu ya Nairobi, ili kuzuia “mienendo hii ya kuwatisha wabunge kupitisha maamuzi ya kidikteta.”

Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Benjamin Washiali alimshtumu Rais kwa kuendesha chama cha Jubilee kama biashara ya mtu binafsi.

Alisema Rais alipuuza utaratibu wa uongozi wa chama pamoja na kamati na baraza la usimamizi wa chama katika kutekeleza mabadiliko kwa chama.

Hata hivyo, kipengee cha 9.1 cha Katiba ya Jubilee kinampa kiongozi wa chama mamlaka ya kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa chama wakati wowote. Na mwaliko wa mkutano wa Jumatatu ulitolewa na Rais Kenyatta mwenyewe.

Bw Murkomen amekuwa akishikilia nafasi hiyo tangu 2017 huku naibu aliyeteuliwa jana seneta wa Isiolo, Bi Fatuma Dullo,amekuwa akishikilia wadhifa huo kwa miaka miwili sasa.

Mkutano huo wa Ikulu ulihudhuriwa na maseneta 20 kati ya jumla ya maseneta 35 wa mrengo wa Jubilee.

Kwenye taarifa iliyotumiwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Ikulu Kanze Dena Mararo, Rais aliwapongeza viongozi wapya wa Jubilee katika Seneti na akawahikikishia kuwa atawaunga mkono.

“Rais ambaye pia ni kiongozi wa Muungano wa Jubilee anataraji kufanya kazi kwa karibu na uongozi mpya wa seneti katika utoaji huduma kwa Wakenya,” akaongeza.

Shoka liliwaangukia Murkomen na Bi Kihika kwa sababu wamekuwa wakosoaji wakuu wa serikali ndani na nje ya Seneti, hali ambayo inasemekana kumkera Rais Kenyatta.

Kwa mfano, juzi Bw Murkomen alipinga hatua ya kupelekwa kwa wanajeshi wanne kuhudumu katika Kaunti ya Nairobi chini ya mwavuli wa afisi ya Nairobi Metropolitan Services (NMS).

Naye Bi Kihika alipinga kufurushwa kwa zaidi ya familia 5,000 kutoka kitongoji cha Kariobangi Sewerage akiitaja serikali ya Rais Kenyatta kama “dhalimu na isiyojali masilahi ya wanyonge.”