Habari

Uhuru akosa njia Kibra

October 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

MGAWANYIKO katika chama cha Jubilee kuhusu uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra pamoja na handisheki zimemuacha Rais Uhuru Kenyatta ‘amechanganyikiwa’.

Ingawa Rais Kenyatta alikutana na mgombeaji wa chama hicho kwenye uchaguzi huo Macdonald Mariga katika Ikulu na kumvisha kofia ya Jubilee, matamshi ya wanasiasa walio karibu naye yanaonyesha amechanganyikiwa kuhusu anayefaa kuunga mkono kwenye uchaguzi huo.

Kinyume na sheria ya vyama vya kisiasa, baadhi ya wabunge wa Jubilee wametangaza wazi kuwa hawatamuunga mkono Bw Mariga mkono wakidai wana baraka za Rais Kenyatta kumuunga mgombeaji wa cha ODM, Imran Okoth

Mnamo Jumapili, mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini, Dennis Waweru waliongoza kampeni za Imran.

“Chama chetu cha Jubilee kimemsimamisha mgombeaji lakini roho ya Rais Kenyatta haiko huko. Roho ya Rais Kenyatta iko kwa Imran Okoth,” akasema Bw Kamanda.

Wanachama wa Jubilee wanaompiga debe Bw Mariga wanadai kuwa wanaomuunga mkono wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto walitumia njia za mkato ili kuhakikisha Rais amemuidhinisha kama mgombeaji wa chama tawala kinyume na mapenzi yake.

Kulingana na Waziri Msaidizi Rachel Shebesh, ambaye amejiunga na wanaomuunga mkono Bw Imran, Rais Kenyatta hakuwa na nia ya kumuidhinisha Bw Mariga.

“Mimi nilikuwa Ikulu wakati huo na ninajua presha aliyowekewa Rais ili kupigwa picha akimuidhinisha Bw Mariga,” Bi Shebesh alidai alipokutana na makundi ya wanawake mtaani Kibra kuwataka wampigie kura Bw Imran.

Japo kanda yake akitoa kauli hiyo ilisambazwa mitandaoni na kuibua hisia kali, Ikulu ya Rais Kenyatta haikukanusha madai yake.

Huku hayo yakijiri, Dkt Ruto amekuwa msitari wa mbele kumpigia debe Bw Mariga na kusisitiza kuwa ana baraka za kiongozi wa chama ambaye ni Rais Kenyatta.

“Si mlimuona kiongozi wa chama akimvisha kofia mgombeaji wa chama? Sasa hawa watu wanataka waambiwe nini kingine,” aliuliza Dkt Ruto akiwasuta wanaodai kuwa Bw Mariga ni mradi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ katika Jubilee.

Kujitolea

Kulingana na wadadisi, Rais Kenyatta hakutaka Jubilee kusimamisha mgombeaji Kibra ili kuonyesha kujitolea kwake katika handisheki yake na Bw Raila Odinga, lakini baada ya chama kumkabidhi tiketi alijipata katika hali ya kuchanganyikiwa na ikabidi akubali.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth aliyekuwa mbunge wa ODM, na kakake Imran.

Alipomuidhinisha Bw Mariga, viongozi wa ODM walitilia shaka kujitolea kwa Rais Kenyatta katika handisheki na baadhi wakamtaka Bw Odinga kuwa mwangalifu.

Hata hivyo mambo yalitulia Bw Kamanda alipokutana na Bw Odinga na kutangaza kuunga mkono Bw Imran “kama mgombeaji wa handisheki.”

Wanaompinga Bw Mariga wanalaumu wanaomuunga mkono kwa kutaka kuvunja handisheki.

Katibu mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju mnamo Jumanne alisema hawana mipango ya kuwaadhibu wanaofanyia kampeni mgombezi wa chama pinzani.