Uhuru apigwa breki na mahakama
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Kuu Alhamisi zilizuia Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuendelea kutekeleza mipango miwili ambayo ni muhimu kwa utawala wa Jubilee.
Katika kesi ya kwanza, korti iliharamisha hatua ya Serikali Kuu kuchukua baadhi ya majukumu ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi.
Mahakama pia ilisema Serikali Kuu ilikosea kwa kuhamisha wafanyakazi 6,052 kutoka Kaunti ya Nairobi na kuwapeleka kwa Idara ya Kusimamia Huduma Nairobi (NMS) inayosimamiwa na Meja Generali Mohammded Badi chini ya Afisi ya Rais.
Na katika kesi ya pili, mahakama kuu imesitisha kwa muda agizo la Serikali kwamba bidhaa zote zinazopelekwa hadi mataifa ya Uganda, Rwanda na Sudan Kusini kutoka bandari ya Mombasa zisafirishwe kwa njia ya reli (SGR) hadi bandari ya nchi kavu iliyo Naivasha.
Usimamizi wa huduma muhimu za Kaunti ya Nairobi ulitwaliwa kutoka kwa Gavana Mike Sonko mnamo Februari 25, 2020, alipotia sahihi makubaliano na Serikali Kuu.
Huduma zilizotajwa ni Afya, Uchukuzi, Ujenzi, na Mipango. Hata hivyo, Serikali Kuu imeonekana kusimamia huduma zaidi ikiwemo ukusanyaji fedha katika kaunti hiyo.
Jaji Hellen Wasilwa alisema shughuli hiyo ilikiuka katiba kwani haikujumuisha maoni ya wananchi.
Aliipa Serikali Kuu muda wa siku 90 kurekebisha dosari hiyo. Muda huo ukitamatika kabla ya marekebisho kutekelezwa, basi Kaunti ya Nairobi itahitajika kurejelea usimamizi wa huduma zake.
Agizo hilo ni ushindi kwa Gavana Sonko aliyelalama kortini kwamba hakuidhinisha uhamisho wa wafanyakazi wake, na wala hakushauriana na NMS kuhusu hatua hiyo.
Jaji Wasilwa alisema bunge la Kaunti ya Nairobi lingelijadili suala hilo na kulipitisha kabla ya wafanyakazi kuhamishwa.
Katika ushahidi aliotoa kortini, Bw Sonko alisema shughuli ya kuhamishwa kwa wafanyakazi ilitekelezwa na maafisa wachache ambao hawakupata ushauri wake wala kusaka maoni ya umma.
Jaji huyo alisema kuwa bodi inayosimamia utoaji huduma katika Kaunti ya Nairobi (NCCPSB) haikushirikishwa kabla ya wafanyakazi hao kuhamishwa.
Kulingana na Jaji Wasilwa, utendakazi katika Kaunti ya Nairobi haukuwa unaendelezwa moja kwa moja na Bw Sonko bali unashirikisha bunge la Kaunti ya Nairobi, kwa hivyo madiwani wangehusishwa kabla ya kuhamisha wafanyakazi.
Hatua ya Serikali Kuu kutwaa baadhi ya majukumu ya Kaunti ya Nairobi ilipingwa mahakamani na mwanaharakati Okiya Omtata, na kuungwa mkono na Gavana Sonko pamoja na bodi ya utoaji huduma katika kaunti hiyo.
Mawakili Henry Kurauka, akimwakilisha Sonko, na Prof Tom Ojienda, akitetea NCCPSB, walieleza mahakama kwamba haki za wafanyakazi hao zilikiukwa kabisa walipotakiwa kujaza fomu ili waajiriwe upya kazini.
“Baada ya kuchambua ushahidi uliowasilishwa na walalamishi na kusoma kwa mapana na marefu stakabadhi pamoja na sheria, nimefikia uamuzi kuwa sheria haikufuatwa kabla ya kuhamisha huduma za wafanyakazi hawa. Shughuli hiyo imeharamishwa, inakinzana na sheria na katiba,” alisema Jaji Wasilwa.
Bw Omtata alikuwa ameshtaki NMS, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), NCCPSB na Mwanasheria Mkuu miongoni mwa maafisa wengine wa serikali.
Katika taarifa aliyotoa mahakamani, Bw Sonko alisema majukumu yote ya usimamizi wa Kaunti hii ya Nairobi yamo mikononi mwa mawaziri wa serikali ya kaunti yake kikatiba.
Alisema Serikali ya Kaunti ya Nairobi na zile nyingine ziko huru na hazihudumu chini ya maelekezo ya mtu yeyote ama idara yoyote.
Kwingineko, amri ya kuzuia usafirishaji bidhaa kwa SGR kutoka Mombasa hadi Naivasha ilibadilishwa na Jaji Pauline Nyamweya wa Mahakama Kuu iliyo Nairobi.
Kesi hiyo pia ilikuwa imewasilishwa mahakamani na Bw Omtatah. Iliratibishwa kuwa ya dharura na Bw Omtatah akaamriwa amkabidhi Waziri wa Uchukuzi James Macharia nakala za kesi hiyo ili ajibu madai kwamba alikaidi na kukiuka sheria.
Bw Omtatah anadai agizo hilo la Waziri linaathiri wafanyabiashara wengi watakaowajibika kugharimika mara mbili kabla ya bidhaa wanazosafirisha kufika kule zinakohitajika.