Uhuru: Mimi si mtu wa kutishwatishwa na yeyote
Na LEONARD ONYANGO
NI nani huyo anayethubutu kumtisha Rais wa Jamhuri ya Kenya? Swali hili limeibuka kufuatia matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe Jumatano aliposema kuwa hatakubali wale wanaomtisha tisha kuendelea kufanya hivyo.
Alisema hayo katika uwanja wa Jacaranda, eneobunge la Embakasi Mashariki, wakati wa utoaji wa hatimiliki 50,000 za mashamba kwa wakazi wa Nairobi.
“Mtu asifikirie kwamba mimi ni mtu wa kutishwa tishwa huku na huko! Kama ni vitisho tutaona vitisho vitazidi upande wa nani. Mimi si mtu wa kutishwa!”
Matamshi hayo yamewaacha wengi na maswali kuhusu alikuwa akizungumzia kumhusu nani.
Baadhi wanasema alilenga washirika wa karibu wa Naibu Rais William Ruto ambao wamekuwa wakimshinikiza kutangaza wazi iwapo atamuunga mkono kiongozi huyo katika kinyang’anyiro cha urais 2022.
Wadadisi wanasema washirika hao wanaonekana kutoa vitisho kwa msingi kuwa walimuunga mkono Rais Kenyatta kuchaguliwa mara mbili, na hivyo anafaa kurudisha mkono kwa kusimama na Bw Ruto, la sivyo wanaweza kuondoa uungaji wao kwake.
Kuna wengine wanaosema alilenga Gavana Sonko, ambaye majuzi ameonekana kujaribu kutisha Rais hasa alipomteua wakili Miguna Miguna kuwa naibu wake, huku akifahamu kulikuwa na mvutano baina yake na Serikali.
Hatua hiyo ilionekana kama vitisho kwa Rais Kenyatta ikizingatiwa Bw Miguna amekuwa mwiba kwa utawala wake, Serikali inashikilia si raia wa Kenya na pia Jubilee inathibiti bunge la Kaunti ya Nairobi, na kwa kumteua ni kama alilenga kumuudhi Rais.
Alichukua hatua hiyo kufuatia matukio ambayo yalionekana kumkasirisha ikiwemo kukamatwa kwa mwandani wake Simon Mbugua na kupunguziwa walinzi.
‘Tuko nyuma yako Rais’
Hapo Jumatano, Bw Sonko alionekana kutambua hili aliposema: “Usiwe na wasiwasi Bwana Rais, tuko nyuma yako, mambo ya Miguna Miguna yasikutishe,” alisema Sonko.
Bw Sonko pia amekuwa akishambulia baadhi ya maafisa wakuu Serikalini wanaoaminika kuwa wandani wa Rais Kenyatta akiwemo Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho.
Rais pia kwa mara nyingine aliwakemea wakosoaji wa mwafaka baina yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kusisitiza kuwa ataendelea kushirikiana naye kwa lengo la kuunganisha Wakenya.
“Wengi walinishutumu nilipoamua kufanya kazi na Raila. Bw Raila ni Mkenya na niko huru kuongea na mtu yeyote. Kazi yetu ni kuunganisha nchi na nitaendelea na msimamo huo,” akasema Rais Kenyatta.
Rais Kenyatta hapa huenda alikuwa akiwalenga wandani wa Naibu Rais ambao wamekuwa wakidai kuwa Bw Odinga analenga kugawanya chama cha Jubilee.
Washirika hao wa Bw Ruto wamekuwa wakidai kuwa mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unalenga kusambaratisha ndoto ya Naibu wa Rais kuingia Ikulu 2022.
Rais Kenyatta na Bw Odinga, hata hivyo, wamekuwa wakisisitiza kuwa mwafaka wao hauna ajenda fiche kuhusiana na siasa za 2022.
Hapo jana, Rais Kenyatta alitaja wanaopinga mwafaka huo kuwa watu wanaoendeleza siasa duni.
Madai ya Sonko
Gavana wa Nairobi Mike Sonko pia alijipata pabaya baada ya kudai kuwa amekuwa akiandamwa na baadhi ya wakuu serikalini.
Gavana Sonko pia alidai kuwa maafisa wakuu serikalini wamekuwa ‘wakidanganya’ rais kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
“Serikali ya kaunti ya Kaunti ya Nairobi imetengeneza na kukarabati jumla ya barabara 15 tangu nilipoingia afisini. Kadhalika, tumeanza ujenzi wa kituo cha kisasa cha zimamoto.”
“Ulifaa kuzindua kituo hicho leo lakini watu wako serikalini waliondoa katika ratiba ya leo kwa sababu wanataka nionekane kwamba sifanyi kazi,” Bw Sonko akaambia Rais Kenyatta.
Gavana Sonko pia alimtaka rais kutoshtushwa na uamuzi wake wa kuteua wakili Miguna Miguna kuwa naibu wake.
Lakini Rais Kenyatta alitaja madai hayo ya Bw Sonko kuwa ya ‘utoto’.
“Lengo langu ni kuboresha maisha ya Wakenya na sina wakati wa kushiriki katika porojo na siasa za kitoto,” akasema Rais Kenyatta.
Kiongozi wa nchi, hata hivyo, aliahidi kushirikiana na Gavana Sonko kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Nairobi.