Waiguru na Karua wabanana mahakamani
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ameonekana kuwa na nia ya kutumia njia ya mkato kutetea ushindi wake hata baada ya Mahakama ya rufaa kuamuru kesi ya kupinga uchaguzi wake isikizwe upya.
Mnamo Jumanne Bi Waiguru aliiomba Mahakama ya Juu itangaze kwamba muda wa kusikiza kwa kesi za kupinga uchaguzi umeisha na kwamba agizo la Mahakama ya Rufaa limepitwa na wakati.
Lakini Bi Karua aling’amua lengo lake na kuwaeleza Jaji Mkuu (CJ) David Maraga na wenzake Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u watupilie mbali ombi hilo na kuamuru kesi iendelee kama ilivyoagizwa.
“Kesi niliyowasilisha haikusikizwa hata!,” Bi Karua alisema kupitia kwa wakili wake Bw Gitobu Imanyara.
Katika ombi lake Bi Waiguru anasema katiba imeweka muda wa kuamua kesi zinazotokana na uchaguzi kuwa miezi sita.
Aliwaomba majaji hao wapitishe kwa kauli moja ya kwamba muda uliopeanwa na katiba wa kuamua kesi zinazotokana uchaguzi mkuu umeisha na kuendelezwa kwa kesi ni kukaidi Katiba.
Bi Waiguru alieleza majaji hao watano kwamba Katiba imeweka muda wa miezi sita wa kukamilisha kesi zote za kupinga walioshinda.
Msimamo huo huo pia ulichukuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyosema kwamba muda ushakamilika.
Lakini wakili Gitobu Imanyara anayemwakilisha Bi Karua alitofautiana na Bi Waiguru na IEBC akisema kesi ya Bi Karua haikusikizwa kwa vile Jaji Lucy Gitari wa Mahakama Kuu ya Kerugoya alimnyima fursa ya kuwasilisha ushahidi.
Hata hivyo, Jaji Gitari alitupilia mbali kesi ya Bi Karua na kumwamuru alipe gharama ya Sh10 milioni.
Majaji wa Mahakama ya Rufaa Mohammed Warsame, Daniel Musinga na Prof Otieno Odek waliamuru kesi hiyo isikizwe upya na Bi Karua akubaliwe kuwasilisha ushahidi.
Majaji hawa walitupilia mbali uamuzi wa Jaji Gitari na kuagiza Bi Waiguru amlipe Bi Karua Sh2milioni gharama za kesi hiyo.
Bw Imanyara alisema kesi hii ya kupinga ushindi wa Bi Waiguru sio mpya kwani ni ile ile tu ya kwanza ambayo haikusikizwa.
“Muda wa miezi sita uliowekwa na katiba haujakamilika kwa upande wa Bi Karua ambaye hakusikizwa,” alisema Bw Imanyara.
Wakili huyu mtajika aliomba mahakama izingatie sheria za uchaguzi na katiba kwa pamoja na kufikia uamuzi kwamba kesi ya Bi Karua ingali jinsi alivyoiwasilisha Septemba 2017.