Waliotafuna mabilioni ya NYS kuanza kukamatwa
Na VALENTINE OBARA
WAHUSIKA wakuu kwenye sakata ya ufisadi katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) wanatarajiwa kuanza kukamatwa na kufikishwa kortini wiki hii.
Hii ni baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inayosimwamiwa na Bw George Kinoti kukamilisha sehemu ya uchunguzi wake na kuwasilisha faili 10 za upelelezi kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) inyoongozwa na Bw Noordin Haji (pichani), usiku wa kuamkia Jumapili.
Upelelezi umekuwa ukilenga kampuni na watu binafsi wapatao 40 wakiwemo maafisa wakuu serikalini wanaoaminika kuhusika katika ufujaji wa karibu Sh9 bilioni za NYS.
“Kikundi cha viongozi mahiri wa mashtaka wakiongozwa na DPP wanakagua faili hizo kwa mara ya mwisho. Faili hizo zilizowasilishwa na DCI ni za awamu ya kwanza ya upelelezi,” afisi ya Bw Haji ilisema jana.
Iliongeza, “DPP anahakikishia umma kwamba hatua mwafaka zitachukuliwa kwa kuzingatia uchanganuzi wa ushahidi haraka iwezekanavyo.”
Ufichuzi wa ufisadi katika NYS uliibua upya mjadala kuhusu jinsi wahusika katika sakata nyingi za miaka ya awali walivyoepuka adhabu kisheria, hali inayosemekana husababishwa na kukosekana ushahidi wa kutosha.
Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw James Orengo, alisema viongozi wa upinzani watashtaki wahusika katika sakata hiyo kama serikali itashindwa kuwafikisha mahakamani wiki hii.
“Kuna genge la wahalifu Kenya katika kila shirika la serikali. Kuanzia wiki hii tunataka kuona watu wakifikishwa kortini la sivyo tuchukue hatua kwa wale ambao tunaweza kupata ushahidi dhidi yao,” akasema Seneta hiyo wa Siaya.
Bw Orengo alimwondolea lawama Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, kwa kimya chake kuhusu sakata hiyo na kusema alitabiri hayo yote zamani na kuambia Wakenya wazi.
Huku hayo yakijiri, mashirika ya kijamii yamepanga maandamano kitaifa kushinikiza serikali kuangamiza zimwi la ufisadi nchini.
Shirika lisilo la kiserikali la National Youth Sector Alliance (NYSA) jana lilitoa wito kwa vijana kuungana kuangamiza ufisadi kwani ndio chanzo cha changamoto zinazowakumba ikiwemo ukosefu wa nafasi za kutosha za ajira.
Mwenyekiti wa shirika hilo, Bw Emmanuel Ngongo, alisema ni lazima serikali ieleze jinsi wahusika katika sakata zote za ufisadi wataadhibiwa na jinsi pesa zilizoibiwa zitarudishwa kwa umma.
“Ni lazima serikali idhihirishe imejitolea kikamilifu kupambana na ufisadi kwa kuadhibu wahusika wakuu badala ya wale wadogo wanaotumiwa kwa ufujaji. Katika sakata iliyopita ya NYS wapelelezi walilenga watu wadogo badala ya wahusika wakuu ndiposa hapakuwa na mafanikio kuwashtaki,” akasema Bw Ngongo.
Maandamano ya wananchi Nairobi yanatarajiwa Alhamisi kuanzia katika bustani ya Uhuru Park kuelekea katika bunge la taifa, mahakama ya juu na barabara ya Harambee.