Weta na Mudavadi waapa kusambaratisha ndoa ya Uhuru na Raila
Na DERRICK LUVEGA na JUSTUS OCHIENG’
Kwa ufupi:
- Mudavadi asema Raila ni msaliti na kama jamii ya Waluhya inafaa kuepukana kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee
- Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”
- Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila
- Ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa
VINARA wa NASA kutoka jamii ya Waluhya sasa wametangaza vita vikali vya kisiasa dhidi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kuwataka wafuasi wao kukataa chama hicho kuelekea uchaguzi wa 2022.
Wakihutubia mikutano ya hadhara katika vituo kadha vya kibiashara kaunti ya Vihiga, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi, walisema Bw Odinga ameikosea heshima jamii ya Waluhya kwa kuisaliti na kuitelekeza.
Walitaja kuondolewa kwa Bw Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti na wao kutajwa kama waoga kama ishara tosha kuwa ODM imetelekeza jamii ya Waluhya.
“Mliona vile alituhepa na kwenda kuzungumza na Uhuru Kenyatta. Na juzi mliona alivyochochea kuondolewa afisini kwa ndugu yangu Weta kama kiongozi wa wachache katika seneti.
Huyo ni msaliti na sisi kama jamii ya Waluhya tuepukane kabisa na chama chake kinachoshirikiana na Jubilee,” Bw Mudavadi akawaambia wafuasi wake mjini Mbale bila kumtaja Bw Odinga kwa jina.
Aliandamana na wabunge, Alfred Agoi (Sabatia), Ernest Ogesi (Vihiga), aliyekuwa seneta wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale, Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka miongoni mwa wengine.
Nao viongozi wa ODM wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, waliwajibu kwa kupuuzilia mbali malalamishi yao.
“Watu wanafaa kuungana kwa masuala yenye umuhimu kwa wananchi kama vita dhidi ya umasikini unaowazonga watu wetu.
Sio masuala potovu kama kuwashambulia wanasiasa wengine,” akasema Bw Sifuna.
Naye Bw Wandayi akasema: “Hakuna aliyeisaliti jamii ya Waluhya. Hakuna mwanasiasa aliye na uwezo kama huo. Hili suala la mabadiliko ya uongozi katika seneti linashughulikiwa na maseneta wenyewe, haifa kutumiwa kumchafulia jina kinara wetu Bw Odinga”.
Kusambaratisha ndoa
Na akiongea mjini Chwele awali, Bw Wetang’ula alisema yeye na vinara wengine wa NASA watafanya juu chini kusambaratisha ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM.
Bw Wetang’ula alimsuta kwa kumsaliti yeye pamoja na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi akisema: “tumeungana ili kukufunza adabu”.
Migawanyiko imekuwa ikitokota katika muungano wa NASA baada ya Bw Odinga kukutana na Rais Uhuru Kenyatta kwa mazungumzo Machi 9 bila kuwahusisha vinara wenzake.
Akiwahutubia walimu katika kituo cha kibiashara cha Chwele wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha ushirika cha Ngarisha, Bw Wetang’ula alisema uamuzi wa Bw Odinga kukutana na Rais bila kuwafahamisha na kuondolewa kwake kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti ni usaliti “ambao hauwezi kuvumiliwa”.
Kulipiza kisasi
“Licha ya sisi kupambana kwa bidii na baadhi ya watu kupoteza maisha yao, mienendo ya mgombea wetu wa urais inashangaza na inaashiria usaliti wa kiwango cha juu,” akasema Bw Wetang’ula huku akiapa kulipiza kisasi.
Alisema ingawa yeye, Mudavadi na Kalonzo wamekuwa wakihimiza kuandaliwe mazungumzo ya kitaifa, utaratibu ufaao haukutumika kuanzisha mchakato huo.
Bw Wetang’ula alisema ni makosa kwa chama cha ODM kuendelea kueneza propaganda kwamba vinara watatu walikwepa sherehe ya kuapishwa kwa Raila mnamo Januari 30.
Alisema ni Raila mwenyewe aliyewashauri kutohudhuria halfa hiyo katika bustani ya Uhuru, Nairobi, ili waweze kumtetea endapo angekamatwa.
“Ni Raila aliyetushauri kukaa kando, kwa hivyo ni makosa kwa wanachama wa ODM kututaja kama waoga kwa kutohudhuria sherehe hiyo ambayo kwa kweli haikuwa na maana,” Bw Wetang’ula akasema.
Fisi
“Kama fisi anataka kuwala wanawe, kwanza huanza kuwashutumu kwamba wananuka harufu inayofanana na ya mbuzi,” akaeleza kwa mafumbo.
Kiongozi huyo wa Ford Kenya alisema yeye na wenzake hawatakubali kutolewa kafara na Raila, akisema wamejipanga kukabiliana naye na Rais Kenyatta bila woga.
“Sasa hafai kujihushisha na masuala ya NASA. Aelekeze nguvu zake katika ushirikiano kati yake na Jubilee na sasa tuko tayari kuendelea na ajenda za upinzani,” Bw Wetang’ula amasema.
Seneta huyo alisema ingawa Bw Odinga amekuwa akidhani kuwa washindani wake wake wako ndani ya Jubilee, atashangaa atakapogundua kuwa vinara wa NASA ambao amewasaliti ndio watammaliza kisiasa.
“Kondoo amekuwa na wasiwasi kuhusu mbwa mwitu kwa miaka mingi lakini aliishia kuliwa na mchungaji,” Wetang’ula akasema.