HabariSiasa

William Ruto hafai kuwa rais – Karua

November 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

Kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua amepuuza azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022 akisema Bw Ruto ‘haungiki mkono’ na kwamba, kati ya watu wote wenye nia ya kutafuta urais 2022, ndiye ‘asiyefaa zaidi.’

Hii ni licha ya viongozi kadhaa kutoka eneo la Mlima Kenya kuunga mkono azma ya Bw Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikiapo 2022.Matamshi hayo makali yanaonyesha mpasuko wa kisiasa eneo la Kati, haswa ikizingatiwa kuwa mbeleni kumekuwa na ishara huenda eneo hilo likamtaliki kisiasa Bw Ruto.

“Ni kweli msimamo wangu ni kuwa, William Ruto ndiye asiyestahili kabisa kwa kazi hiyo (ya urais) na kwa sababu hiyo, sitawahi kumuunga mkono. Wanaoendesha kampeni zake wakome kuhusisha jina langu,” Bi Karua alisema kwenye akaunti yake ya Twitter Novemba 13, baada ya madai kuibuka kuwa anamuunga Bw Ruto mkono.

Haikuwa mara ya kwanza kwa Bi Karua kueleza wazi uhasama wake wa kisiasa dhidi ya Ruto, hata mbeleni wawili hao hawakuwa wakionana macho kwa macho.

“Kuunga mkono watu wasioungika si kati ya mpango wangu. Afadhali niwe nje na sisubiri kuelekezwa na mtu yeyote,” Bi Karua akasema Alhamisi.

 

Mlima wa kupanda

Kauli ya Bi Karua inadokeza wazi kuwa Ruto bado ana kibarua kigumu kudhihirisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya, haswa kufuatia visa vya viongozi wenye ushawishi eneo hilo kumpiga vijembe na kusema eneo hilo halimtambui.

Vita hivi vimekuwa vikiendelea mitandaoni, baada ya kikundi kinachojiita ‘Team William Ruto’ kwenye Twitter kumtaja Bi Karua kuwa ‘yatima wa kisiasa’ kikimtaka adumishe vita vyake vya kisiasa kwa kiwango cha Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru badala ya kumshambulia Naibu wa Rais.

Bi Karua sasa ni miongoni mwa wanasiasa kadhaa kutoka Mlima Kenya ambao wamemtaka Bw Ruto awe tayari kwa makabiliano makali ya upinzani itakapofika 2022. Miongoni mwa viongozi hao ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo ambaye alikuwa kati ya viongozi wa kwanza zaidi kumweleza naibu wa Rais kuwa asidhani ataungwa mkono kiholela na watu wa eneo hilo.

Vilevile, Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu mara kwa mara amekuwa akimshambulia Bw Ruto kupitia kampeni zake za #Kitaeleweka, ambapo amekuwa akisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya linashughulika na kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kufanikisha malengo yake ya maendeleo na wala si kupiga kampeni za naibu wa Rais kuingia ikulu 2022.

Kuhusu suala la eneo la Bonde la Ufa kudai wenyeji wa Mlima Kenya wanafaa ‘kuwarudishia mkono’, Bw Wambugu amekuwa mstari wa mbele kuhubiri kuwa ‘hatutauziwa woga’, kwa maana kuwa kambi ya Bw Ruto haitafanikiwa kushurutisha jamii ya Mlima Kenya kumuunga mkono kwa nguvu.