Habari za Kitaifa

Ikulu yaomba Sh1.7 bilioni kufidia wafanyakazi wa Afisi ya Mke wa Rais

Na SAMWEL OWINO July 19th, 2024 1 min read

IKULU inataka irejeshewe Sh1.7 bilioni kati ya Sh5 bilioni zilizokatwa ili kuiwezesha kuwalipa wafanyakazi wa ofisi iliyovunjwa ya Mke wa Rais Rachael Ruto.

Msimamizi wa Ikulu, Katoo Ole Metito jana aliwaomba wabunge kufikiria kurejesha angalau Sh1.7 bilioni, ambazo zinajumuisha Sh591 milioni zilizokusudiwa kuwalipa wafanyakazi katika afisi ya mke wa Rais.

Licha ya kuvunjwa kwa afisi hiyo na Rais William Ruto kama sehemu ya hatua za kubana matumizi baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, Bw Ole Metito aliwaambia wabunge kwamba wafanyakazi hao walikuwa na kandarasi ambayo serikali inapaswa kuheshimu.

Bw Ole Metito alipofika mbele ya kamati ya utawala na Usalama wa Ndani kuhusu makadirio ya ziada ya bajeti, alisema baadhi ya wafanyakazi katika ofisi hiyo wana kandarasi ya miaka mitatu huku wengine wakiwa na kandarasi ya miaka mitano na hivyo ni lazima walipwe fidia hata ikiwa ofisi hiyo ilivunjwa.