Jamvi La Siasa

Jinsi Bassirou Faye alivyolala ‘maskini’ na kuamka akiwa tajiri

March 30th, 2024 2 min read

MASHIRIKA Na WANDERI KAMAU

USHINDI wa rais mteule wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ni sawa na mtu kulala maskini na kuamka akiwa tajiri.

Siku 10 kabla ya uchaguzi huo kufanyika, alikuwa mfungwa.

Naam, alikuwa akitumikia kifungo gerezani, pamoja na aliyekuwa kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko.

Hata hivyo, ushindi wake Jumapili ilyopita, ambapo alipata asilimia 54 ya kura kwenye uchaguzi huo, umetajwa na raia wengi wa Senegal kuwa wa kimiujiza.

Mwaniaji wa muungano tawala wa taifa hilo-Benno Bokk Yakaar- Amadou Ba, alizoa asilimia 36 ya kura. Mwaniaji huyo alikuwa akiungwa mkono na rais anayeondoka, Macky Sall.

Faye aliwania urais kwa tiketi ya chama cha Pastel, kinachoungwa mkono na Sonko.

“Huu ni ushindi wa kimiujiza. Ni ushindi ambao umedhihirisha kuwa raia wa Senegal walikuwa wamechoshwa na ukatili uliokuwa ukiendelezwa na utawala wa Macky Sall dhidi ya viongozi wa upinzani,” akasema Abdul, ambaye ni mkazi wa jiji kuu la taifa hilo, Dakar.

Kulingana na wadadisi, Sonko ndiye alichangia pakubwa ushindi wa Faye, kwani kulingana na mpangilio wa chama cha Pastel, Sonko ndiye alikuwa amepangiwa kuwania urais kwa tiketi yake.

Hata hivyo, Faye alilazimika kuwania baada ya Sonko kuzuiwa kuwania.

Faye, ambaye hajawahi kuhudumu serikalini hapo awali, ameahidi kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi katika taifa hilo la eneo la Afrika Magharibi.

“Nitaleta mageuzi kwa manufaa ya raia wote wa Senegal. Nitawaaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa waliofungwa gerezani bila sababu zozote au kutokana na misimamo ya kisiasa,” akasema Faye.

Kwenye ahadi ya kufufua uchumi wa taifa hilo, Faye amesema kwamba atabuni sera za kurejesha imani kwa wawekezaji kutoka nje.

Wadadisi wanafananisha ushindi wa Faye sawa na ushindi aliopata Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki mnamo 2002 chini ya muungano wa Narc.

Mzee Kibaki alipata ushindi huo, baada ya utawala wa Kanu kuwahangaisha viongozi wa upinzani na wakosoaji wake kwa miaka 24.

“Bila shaka, kuna sadfa nyingi katika ushindi wa Kibaki na Faye, kwani wote waliibuka washindi katika mazingira ambapo tawala zilizokuwepo zilikuwa zikiwahangaisha wakosoaji wake. Macho yote kwa sasa yataelekezwa kwa Faye, kuona ikiwa atatimiza ahadi alizotoa kwa raia,” akasema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za kimataifa.

Fare atalishwa kiapo mnamo Aprili 2, 2024.

Tayari alishakutana na kushauriana na Rais anayeondoka, Sall.