Kimataifa

Jinsi viongozi wa upinzani Tanzania Lissu, Mbowe walinyakwa ‘kuzuia kuiga maandamano nchi jirani’


DAR ES SALAAM, Tanzania

NAIBU mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu na viongozi wengine waliokamatwa juzi wameachiliwa huru, polisi na msemaji wa chama hicho wamesema.

Viongozi hao wa upinzani pamoja na mamia ya wafuasi wao walikamatwa kuanzia Jumapili hadi Jumatatu kuwazuia kuhudhuria mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana mjini Mbeya kusini mwa Tanzania, iliyofanyika Jumanne.

Makundi ya Kutetea Haki za Kibinamu yalilaani kukamatwa kwa viongozi hao, huku Amnesty International ikidai hatua hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za kutisha upinzani kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi wa kitaifa 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan amechukua hatua za kulegeza udhibiti wa vyombo vya habari na upinzani tangu alipoingia mamlakani 2021, lakini makundi ya kutetea haki yanasema visa vya wakosoaji wa serikali kukamatwa na kuzuiliwa kiholela vimeendelea kushuhudiwa.

Polisi walipiga marufuku mkutano ambao kundi la vijana wa CHADEMA lilipanga kufanya kwa misingi kuwa “ungehujumu amani”.

Kwa ujumla zaidi ya wafuasi 500 wa chama hicho cha upinzani walikamatwa akiwemo mwenyekiti wao Freeman Mbowe kuanzia Jumapili hadi Jumatatu.

“Hatuwezi kutoa nafasi kwa wahalifu wachache kuvuruga amani kwa kuiga yale yanayofanyika katika mataifa jirani,” kamishna wa polisi Awadh Haji alisema Jumatatu jioni.

Alionekana kurejelea maandamano ya vijana wa Gen Z, yaliyofanya nchini Kenya kuanzia Juni na kuchochea maandamano mengine katika nchi za Nigeria na Uganda.

Mnamo Jumanne jioni, Msemaji wa CHADEMA John Mrema alithibitisha kuwa viongozi wakuu wa chama hicho waliachiliwa huru.

Hata hivyo, kulikuwa na ripoti kwamba baadhi ya vijana wakeretetwa wa chama hicho mjini Mbeya bado walikuwa wanazuiliwa.

Sarah Jackson, naibu mkurugenzi wa shirika la Amnesty International ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini ameitaka serikali ya Tanzania kukomesha “vitendo vya kukamatwa kiholela na kuzuiliwa kwa viongozi wa upinzani.”