Habari za Kitaifa

Joho: Mimi si mshenzi, nimebadili msimamo wangu na nitamkumbatia Ruto tufanye kazi

Na CHARLES WASONGA August 4th, 2024 1 min read

WAZIRI Mteule wa Wizara ya Uchumi wa Maji, Uchimbaji Madini na Masuala ya Baharini Hassan Ali Joho amepiga abautani na kujitenga na kauli yake ya awali kwamba hangezungumza au kushirikiana kwa njia yoyote na Rais William Ruto.

Akihojiwa Jumapili kubaini ufaafu wake kwa kibarua hicho, Joho alikiri kuwa amebadilisha mtazamo wake kutoka kuwa mkosoaji mkubwa Dkt Ruto, na serikali yake, hadi kufanyakazi naye, kama waziri kuwatumikia Wakenya.

“Ni washenzi pekee ambao huwa hawabadili misimamo yao. Kwa sababu mimi sio mshenzi nimebadili msimamo wangu na sasa niko tayari kuwahudumia raia kama mawaziri chini ya serikali yake. Kimsingi, sote kama viongozi walioko serikali na wale wa upinzani, huwahudumia Wakenya,” akasema.

Bw Joho alikuwa akijibu swali kutoka kwa mwanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi Naisula Lesuuda kujua ni vipi atafanya kazi na Rais Ruto ilhali aliwahi kuapa kwamba hatawahi kufanya kazi naye.

“Umemshukuru Rais kwa kukupendekeza kushikilia wadhifa wa uwaziri na ndio maana u mbele ya kamati hii. Lakini umewahi kuapa kwamba hautawahi kushirikiana wala kuongea na Rais Ruto. Je, sasa utahusiana naye vipi kama waziri katika serikali yake endapo kamati hii itaidhinisha uteuzi wako,” Mbunge huyo wa Samburu Magharibi akamuuliza Joho.

Mnamo Februari 8, 2022 Bw Joho, ambaye alikuwa naibu kiongozi wa ODM, alisema kuwa hakuwa na nia ya kujiunga na kambi ya Dkt Ruto, wakati huo akiwa Naibu Rais.

“Mbona nimtafute Ruto? Ili anipe wilbaro? Sitaki kuhusiana kwa njia yoyote na Ruto. Sitaki kushirikiana na mtu anayenikumbusha kuhusu umasikini,” Bw Joho akanukuliwa akisema akiwa Mombasa.

Jumapili, mwenyekiti wa kamati hiyo Spika Moses Wetang’ula aliunga mkono kauli ya sasa ya Bw Joho kwamba, “ni washenzi pekee ambao huwa hawabadilishi misimamo yao.”