Habari Mseto

Juhudi za viwanda vidogo vya majani chai kuwa huru zaanza kufanikiwa

Na VITALIS KIMUTAI September 22nd, 2024 2 min read

JUHUDI za viwanda vidogo 17 vya Shirika la Ustawi wa Majani Chai (KTDA) kujitenga kutoka viwanda vikubwa zinazaa matunda kwa baadhi ya viwanda hivyo kufuatia kuundwa kwa kamati ya kiufundi kufanikisha mchakato huo.

Aidha, kampuni tatu katika kaunti za Bomet na Kericho zimepewa kibali na serikali kuu kuendesha shughuli zao za kifedha kivyao kufuatia msururu wa maandamano ya wakulima katika eneo hilo.

Viwanda vya Chelal na Toror vimepiga hatua katika juhudi zao za kuwa na akaunti zao tofauti na zile za viwanda vikuu vya Litein na Tegat vilivyoko katika kaunti ya Kericho.

Kiwanda cha majani chai cha Motigo kilichoko katika kaunti ya Bomet ni kiwanda cha kwanza kupata kibali cha kujitenga kifedha na kampuni ya Kapkoros na kampuni shirika za Tirgaga na Olenguruone.

“Tumebuni kamati ya kiufundi kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na viwanda 17 ili tuweza kuyakagua kila moja na kuona ikiwa yana mashiko. Hii itawezesha mchakato huo kuendeshwa kwa utaratibu bila kuvuruga shughuli za kawaida za viwanda,” akasema Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt Paul Ronoh.

“Baada ya kusikiza malalamishi yaliyoibuliwa na wakulima katika kaunti ya Bomet, tutatenganisha kiwanda cha Motigo kutoka kile cha Kapkoros na kukifanya huru, walivyotaka washikadau,” Dkt Ronoh akasema.

Kuundwa kwa kamati hiyo ya kiufundi kunafuatia kufanyika kwa mkutano wa mashauriano kati ya Afisa Mkuu Mtendaji wa KTDA Wilson Muthaura, Mwenyekiti wa Bodi ya KTDA Enos Njeru na maafisa kutoka Bodi ya Majani Chai Nchini (TBK) wakiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Willy Mutai, wiki mbili zilizopita.

Imebainika kuwa idadi kubwa ya viwanda ambavyo havijapewa uhuru wa kusimamia masuala yao kifedha viko Magharibi mwa Bonde- eneo linaloshirikisha kaunti za Bomet, Kericho, Nyamira, Kisii, Nandi, sehemu za Nakuru na Kaunti ya Narok.

Kiwanda kikuu huwa na viwanda vinne kwa wastani chini ya usimamizi wake.

Shirika la KTDA husimamia viwanda 21 vya majani chai katika kaunti 21.

Viwanda 54 kati ya hivyo vinatambuliwa kama asasi huru, lakini vikiwa na viwanda 17 vidogo vinavyosimamia.