Habari za Kitaifa

Jumamosi ni kazi, Mwanasheria Mkuu mpya aagiza wafanyakazi wake

Na KEVIN CHERUIYOT August 22nd, 2024 1 min read

MWANASHERIA Mkuu mpya, Dorcas Oduor, ametangaza mabadiliko yanayolenga kupunguza mrundiko wa kesi ambazo zimechukua miaka mingi kushughulikiwa na afisi yake.

Hatua hiyo, alisema, inalenga kuhakikisha kesi zote ambazo zimechukua miaka mingi zinashughulikiwa.

Na sasa, amewaagiza maafisa katika ofisi yake kufanya kazi Jumamosi kama njia ya kuhakikisha kesi hizo zinashughulikiwa.

“Kuanzia Jumamosi ijayo, tutakuwa tukitoa huduma bila kutoza malipo,” akasema Bi Oduor.

Kulingana naye, kwa muda wa wiki nne za kwanza, maafisa katika ofisi yake watakuwa wakifanya kazi Jumamosi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa saba alasiri ili kuondoa mrundiko.

Pia, ametangaza kuwa wakuu wa idara katika ofisi yake watawezeshwa kushiriki katika mikutano ya hadhara ili kujifahamisha na jamii.

Isitoshe, kuanzia Jumatano wiki ijayo, kutakuwa na mpango mpya uitwao Sheria Space kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi na moja jioni, utakaowawezesha Wakenya kuwafahamu wakuu wa idara kadhaa.

“Tutawatambulisha wakuu wetu wa idara mbalimbali kwa Wakenya na kile tunachofanya. Tutawasikiliza ili tufahamu matarajio yao kutoka kwetu. Tunatumai Wakenya wote watajiunga nasi.”

Katika jukwaa hilo, kila mtu kutoka kwa mfumo wa uhalifu na haki pia atatangamana na wananchi kuhusu jinsi ya kuendeleza maslahi ya umma.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alisema uzoefu wa Bi Oduor utamwezesha kufanya kazi vizuri na maafisa katika kutatua baadhi ya kesi ambazo bado hazijakamilika.

“Ni uteuzi unaofaa sana ambao ninamkabidhi mtu ambaye nina imani naye sana, ambaye nimekuwa nikishauriana naye mara kwa mara,” Bw Muturi alisema.

Alitoa changamoto kwa Bi Oduor kuwapa kipaumbele baadhi ya maafisa ambao wamefanya kazi kwa miaka mingi bila kupandishwa vyeo, akilaumu Tume ya Utumishi wa Umma kwa kukwamisha azma yao ya kupandishwa vyeo.