Habari

Kang'ata adai baadhi ya magavana wamehonga maseneta wapinge mfumo wa ugavi wa pesa

August 24th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MNADHIMU – kiranja wa wengi – katika bunge la Seneti Irungu Kang’ata amesema kuwa hana uhakika wa suluhu la ufadhili wa kaunti kupatikana hivi karibuni akidai baadhi ya magavana wametoa hongo kwa baadhi ya maseneta waendelee kupinga.

Akiongea katika Kaunti ya Murang’a, Kang’ata alilalama kuwa magavana kutoka Kaunti ambazo zinatarajiwa kupunguziwa fedha iwapo mfumo wa kuzingatia idadi ya watu utapitishwa, ndio wametenga vitita vya hongo kwa maseneta.

Alisema kuwa kuna ushahidi wa kuunga mkono hayo, huku akiwa katika shinikizo za kusaidia serikali kupata suluhu la kugawa pesa kwa serikali za Kaunti.

Kang’ata alidai kuwa maseneta hao walafi sasa ndio wanaonekana wakipinga mfumo wa ugavi pesa hizo bila kutoa sababu thabiti.

“Unapata kwamba baadhi ya maseneta wanahudumia kaunti ambazo zitanufaika na nyongeza ya pesa iwapo mfumo wa serikali utapitishwa lakini wanapinga,” akasema.

Aidha, alisema kuwa kuna maseneta wengine ambao wanapinga mfumo uliopendekezwa na serikali wa kuzingatia idadi ya watu “kwa msingi kuwa viongozi wao wa kisiasa wamewaamrisha kufanya hivyo.”

Wengine ni wale ambao wana nia ya kuwania ugavana 2022 na ambapo wanatumia mjadala huo kujipigia debe kama watetezi sugu wa Kaunti zao hivyo basi kukwamiza harakati za kufathili ugatuzi kwa miezi matatu mfululizo sasa.

Katika siku za awali, Kang’ata akichangia mjadala huu wa ugavi wa pesa kwa Kaunti amewalaumu Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto kwa kutowawajibikia kusaidia Rais kupata ushindi wa kura ya mfumo huo katika bunge la Seneti.

Ni hali ambayo tayari imemweka katika hasira ya Rais ambaye alimpigia simu akimkanya dhidi ya kutumia maelewano ya handisheki pamoja na mpango wa uwiano wa kitaifa kuhusu BBI kama silaha za kupigia debe mfumo huo kupitishwa.

Aidha, hafla ya mlo aliyopanga hivi majuzi ya kuwaleta maseneta pamoja ili waelewane kuhusu kura ya mfumo huo ilizimwa ghafla na Ikulu na kumwacha Kang’ata akiwa na chakula na vinywaji bila wa kujivinjari.

Hata hivyo, Kang’ata alisema kuwa serikali haitaondoa mfumo huo kutoka mjadala wa bunge na ndio utazingatiwa hadi kwa kura ya kuamua.

“Huu ni mfumo ambao serikali itazidi kupendekeza katika mijadala yote ijayo ya Seneti. Hatutazingatia mapendekezo ambayo yanatolewa kwa kuwa hayajapitia kwa mashauriano na umma na pia kupata ushauri wa wataalamu. Mfumo tulio nao bungeni umetimiza vigezo vya kisheria kuhusu ushirikishi wa umma na kisha kuandaliwa kama mfaafu zaidi na taasisi husika ambayo ni tume ya ugavi raslimali (CRA),” akasema.

Tayari, bunge la Seneti limeunda kamati ya maseneta 12 ya kujaribu kutatua suala hili ambalo limeishia kutumbukiza kaunti kadha kwa migomo ya wafanyakazi ambao wamekosa mishahara.

Maseneta katika Kamati hiyo ni Moses Wetang’ula wa Bungoma, Johnson Sakaja (Nairobi), Stewart Madzayo (Kilifi), Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika (Nakuru), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Samson Cherargei (Nandi), Moses Kajwang’ (Homa Bay), John Kinyua (Laikipia), Ledama ole Kina (Narok) na Anue Loitiptip (Lamu).

Kwa sasa, matumaini yako kwa kamati hii lakini Kang’ata akilaumiwa kwa kuzingatia msimamo mkali ambao hautoi mwanya wa majadiliano na maelewano.