Habari Mseto

KQ yasaka mkataba kupunguza bei ya mafuta ya ndege

June 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Ndege nchini (KQ) limepanga kuingia katika mkataba wa kulikinga dhidi ya athari za ongezeko la bei ya mafuta ya ndege.

Shirika hilo limepanga kufanya hivyo kabla ya mwisho wa mwaka huu, miaka miwili baada ya kuondoa mkataba kama huo.

Wasimamizi wa shirika hilo wanazungumza na benki na mashirika mengine katika sekta ya kawi kuingia katika mkataba huo.

2017, KQ ilitumia Sh25 bilioni (asilimia 30 ya gharama ya operesheni zake) kununua mafuta ya ndege.

Bajeti ya mafuta inaathiri juhudi za shirika hilo kuimarika kimapato na kutokana na kuwa imekuwa vigumu kubashiri bei ya mafuta, kutatua changamoto hiyo ni jambo la muhimu zaidi kwa KQ alisema Mkurugenzi Mkuu Sebastian Mikosz Ijumaa.

Huenda bei ya mafuta ikaendelea kuongezeka katika siku zijazo, na ndio maana shirika hilo limechukua hatua mapema, baada ya kulemazwa na gharama ya mafuta kwa miaka miwili.