Habari za Kitaifa

Kule Shakahola, kuna waliofunga na kufungwa kamba wakisubiri kifo, video zabaini

Na BRIAN OCHARO July 24th, 2024 2 min read

WAUMINI wa kanisa la mhubiri tata Paul Mackenzie walifungwa kwa kamba wakiwa bado hai wakati wa kutekeleza mfungo na kuzikwa hivyo baada ya kufariki.

Video ya zoezi la ufukuaji wa maiti iliyochezwa katika mahakama ya Shanzu Jumatatu, ilifichua kwamba waliowazika wafuasi wa kanisa la Good News International linalohusishwa na Mackenzie, walihakikisha kwamba hawangetoroka hata katika kifo.

Picha hizo zilionyesha miili hiyo ikiwa imefungwa kwa shuka nyeupe, huku sehemu za mguu na shingo zikiwa zimefungwa kwa kamba. Miili mingine ilikuwa imefungwa kwa blanketi na mifuko ya plastiki.

“Sijawahi kuona kitu kama hiki hapo awali. Nilikuwa nikiitoa miili hiyo kwenye udongo kwa uangalifu baada ya wachimba makaburi kuchimba na kufika eneo ambalo miili hiyo iliwekwa,” alisema Konstebo wa polisi Bernard Jefwa.

Ushahidi wake unatoa uthibitisho kwa uchunguzi wa awali wa polisi unaoonyesha kuwa kulikuwa na vyumba vya mateso ndani ya msitu huo, ambapo vipande vya nguo na kamba, pamoja na vitu vingine vingi ambavyo havikutambuliwa, vilipatikana mwaka jana.

Wapelelezi walisema kuwa katika harakati za kuwatafuta na kuwaokoa baadhi ya wahasiriwa waliokuwa wamefungiwa katika nyumba mbalimbali, walipatikana wakiwa uchi, huku miguu yao ikiwa imefungwa pamoja kwa vitambaa ili kuwazuia kutoroka au kuomba msaada.

Bw Jefwa anafanya kazi katika idara ya kupeleleza mauaji ya binadamu na kazi yake nyingi inahusisha ufukuaji wa miili.

“Nimefukua miili kadhaa kwingine kabla ya tukio la Shakahola. Nilikuwa nimefanya kazi hii kwa miaka miwili kabla ya kuitwa kujiunga na timu nyingine msituni,” alisema alipoulizwa na kiongozi wa mashtaka, Bw Victor Owiti kuhusu kazi na tajriba yake.

Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu, Bi Leah Juma alitazama video iliyokuwa ikionyeshwa kwenye runinga iliyowekwa mahakamani.

Kupitia kwa video hiyo, Hakimu alirejeshwa kwenye mchakato wa uchimbaji wa kaburi uliotokea msituni mwaka jana. Hakimu alitazama picha hizi zinazoonyesha maiti za wahasiriwa walipokuwa wakitolewa kwenye udongo.

Ilikuwa ya kutisha, lakini Hakimu Juma alijizatiti kuitazama huku akiandika.”Kabla ya kutoa miili hiyo kutoka kaburini, ilinibidi kutia alama kila mwili, kuupa namba, kuuweka kwenye begi tofauti na kufunga zipu kusafirishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa upasuaji,” alisema Bw Jefwa.

Kanda zilipokuwa zikionyeshwa kortini, Mackenzie alifuata kwa makini kabla ya kusimama kutoka kwenye kiti chake kumnong’oneza wakili wake, Lawrence Obonyo.

Aliporudi kwenye kiti chake, aliinamisha kichwa chake kwa muda kana kwamba alikuwa katika mawazo mazito kabla ya kukiinua tena kutazama picha za maiti zikitolewa ardhini huku mkono wake wa kushoto ukiegemea kidevuni mwake mara kwa mara.

Katika kesi hii, Mackenzie, mkewe Rhoda Maweu na wengine 93 wamekana makosa manne yanayohusiana na ugaidi na itikadi kali.