Pambo

Kundi la ufundi wa chumbani lashangaza wanaume

January 30th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KULIZUKA kizaazaa katika ukumbi mmoja mjini Nyeri wakati wanaume kadhaa waliuvamia wakilaani hatua ya shirika moja lisilo la kiserikali kuwafundisha wake wao kuhusu ufundi wa masuala ya chumbani.

Wanaume hao walilalamika huku wakisuta hatua hiyo ya muungano unaojiita Operesheni Dumisha Ndoa.

Kundi hilo linalenga familia za eneo la Kati kuzindua misururu ya utoaji wa elimu kwa wanawake ambayo inalenga kuimarisha ubunifu wao wa namna ya kuwatunza waume wao.

Wakuu wa kundi hilo walisema lengo ni kuona kwamba ndoa katika eneo la Mlima Kenya zinasimama tisti, bila kuyumbishwa na tabia za ‘mipango ya kando’.

Shida ilitokea wakati baadhi ya wanawake walioshiriki vikao walipakia picha na video za mafundisho hayo.

“Baadhi ya wanaume wao ambao ni wahudumu wa bodaboda mjini Nyeri waliafikiana kufika katika ukumbi huo kuwasilisha malalamiko yao,” akasema mdokezi aliyezungumza na Taifa Leo.

Wanaume hao walitoa malalamiko kwamba wake wao walikuwa wakichanuliwa jinsi ya kuwa mafundi wa masuala ya chumbani, wakisema ni hatari sana kwa sababu “wako wanaoweza kugeuka viruka njia na wakimbizane na wanaume wazinzi”.

“Ikiwa nia yenu ilikuwa nzuri katika maandalizi ya elimu ya aina hii, basi mlipaswa kutualika sisi waume tujifahamishe na mengi. Binafsi ninahisi ni kosa kualika mke wangu bila kunihusisha,” mwanamume mmoja akalalamika.

Soma Pia: Wanaume wa kupenda ndogondogo watiwa majaribuni kwa kutangaziwa bonasi

Nao wanaume wengine waliogopa wakisema kwamba huenda muungano huo ulikuwa na nia ya kuwasajili wake wao kwa mtandao wa usagaji.

“Itakuwaje wanawake pekee wawe ndio wanaelimisha wanawake wenzao kuhusu ufundi wa masuala ya chumbani? Mbona sisi wanaume tusishiriki kwa kuchangia maoni jinsi ambavyo tungependa mambo yawe? Si mnaona tuko na haki ya kuingiwa na shaka?” akauliza mwanamume mmoja.

Lakini mshirikishi wa harakati za Operesheni Dumisha Ndoa Faisal Wanjiru alisema kwamba kiini kimojawapo cha baadhi ya wanaume kutoka nje ya ndoa na kujiingiza katika uasherati ni wake wao kukosa ufundi wa namna ya kuwatunza waume wao.

“Tuliamua kushughulika na makundi ya kina mama na kuwahami na mbinu za kuwa wake wa kutamanika na waume wao. Hatukutaka waume wao kwenye vikao hivi kwa sababu tulikuwa tunajadili mambo ya kisichana na ambayo yanafaa kubaki kuwa siri. Tulikuwa tunawaibia siri ya kuwateka waume wao ili watulie ndani ya boma,” akasema Bi Wanjiru.