Makala

Kuria, Ababu waongoza orodha ya mawaziri walioachwa nje wakipigwa na kibaridi


RAIS William Ruto hatimaye amewatema kabisa mawaziri 12 wa zamani kwa kufeli kuwateua upya katika baraza lake jipya la mawaziri huku akiwateua tena wenzao 11.

Wao ni; aliyekuwa waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, Aisha Jumwa (Jinsia), Penina Malonza (Ustawi wa Maeneo Kame), Zacharia Njeru (Maji), Simon Chelugui (Ustawi wa Vyama vya Ushirika) na Profesa Njuguna Ndung’u (Fedha).

Wengine walioachwa kwenye baridi ni; Ababu Namwamba (Michezo), Eliud Owalo (ICT), Mithika Linturi (Kilimo), Ezekiel Machogu (Elimu), Susan Nakhumicha (Afya) na Florence Bore (Leba).

Waliokuwa wenzao ambao Rais Ruto amewateua tena ni Aden Duale (Mazingira), Soipan Tuya (Ulinzi), Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Alice Wahome (Ardhi), Kipchumba Murkomen (Vijana), Rebecca Miano (Utalii), Salim Mvura (Biashara), Alfred Mutua (Masuala ya Jamii), Justin Muturi (Utumishi wa Umma) na Davis Chirchir aliyerejeshwa katika Wizara ya Barabara.

Rais Ruto aliwateua mawaziri wapya watano mnamo Ijumaa wiki jana pamoja na watu wengine sita wapya aliowapendekeza kushikilia nyadhifa za uwaziri.

Wao ni pamoja na Debra Mlongo aliyependekezwa kuwa Waziri wa Afya kuchukua mahala pa Bw Nakhumicha, Julius Migos Ogamba aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu kuchukua nafasi ya Bw Machogu na Margaret Nyambura Karanja aliyeteuliwa kuwa Waziri wa ICT kuchukua nafasi ya Bw Owalo.

Wengine ni; Mhandisi Eric Mureithi Muuga aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Maji kuchukua nafasi ya Bw Njeru na Andrew Mwihia Karanja aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo kuchukua nafasi ya Bw Linturi aliyezongwa na sakata za ufisadi.

Katika uteuzi alioufanya Jumatano, Julai 24, 2024, Rais Ruto alimpendekeza Bw John Mbadi kujaza nafasi ya Profesa Ndung’u (Wizara ya Fedha) huku nafasi ya Bw Chelugui ikitunukiwa aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya.

Nayo nafasi Bi Jumwa ilipewa Bi Stella Langat ambaye sio mwanasiasa huku nafasi Bw Kuria ikipewa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi.

Nafasi ya Bw Namwamba imepewa aliyekuwa Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen kupitia uteuzi upya.

Kulingana na orodha mawaziri 10 wateule ambayo Rais Ruto alitoa Jumatano, mawaziri wengine wa zamani aliowarejesha katika baraza lake la mawaziri ni Salim Mvurya alimpendekezwa kuwa Waziri wa Biashara na Bi Rebecca Miano aliyemteua upya kuwa Waziri wa Utalii.

Mwingine ni waziri wa zamai wa Utali Alfred Mutua ambaye Rais Ruto alimpendekeza kuwa Waziri wa Leba.

Wizara ya Uchumi wa Majini iliyoshikiliwa zamani na Bw Mvurya imetununikiwa aliyekuwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho.

Aidha, kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi amependekezwa kuwa Waziri wa Kawi. Wadhifa huo zamani ulishikiliwa na Bw Chirchir ambaye sasa amehamishwa kusimamia Wizara ya Barabara.

Kando na kuwarejesha mawaziri wake 11 wa zamani, wengi wao wakiwa wanasiasa, Ras Ruto pia amewateua wanasiasa wanne kutoka chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Wao ni; Mbw Mbadi, Wandayi, Oparanja na Joho.

Mbw Oparanja na Joho ni manaibu wa Bw Odinga katika ODM na kila mmoja amekuwa akiendesha kampeni ya kurithi kiti hicho.

Hii ni kwa sababu Bw Odinga huenda akajiuzulu wadhifa wa kiongozi wa chama hicho akifaulu kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).