Akili MaliMakala

Kwa nini Kenya ilalamike njaa mifumo ya bayoteknolojia ikiwepo kuzalisha chakula?

Na SAMMY WAWERU September 18th, 2024 3 min read

KUFUATIA mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kushuhudiwa ulimwenguni, Kenya inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi Upembe wa Afrika.

Hii ni kulingana na ripoti ya 2021 ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), ambayo inaonyesha athari kama vile ukame wa muda mrefu, hasa katika maeneo kame (ASAL), mafuriko, wadudu waharibifu, na magonjwa zimechangia hali kuwa mbaya.

Nchini, hali hii ilichochewa kuwa mbaya zaidi na mlipuko wa nzige wa jangwani mwaka wa 2019 hadi 2020.

Licha ya changamoto hizi, ambazo zinaweza kuchukua miongo kadhaa kuangaziwa, wataalamu wa kilimo wanasema umewadia wakati Kenya na Bara la Afrika kwa jumla kukumbatia mfumo wa Bayoteknolojia.

Njia hii itasaidia sana kukabiliana na uhaba wa chakula na njaa, huku serikali ikikaza kamba juhudi zake kwa kulenga usalama wa chakula kupitia Ajenda ya Kuinua Uchumi kutoka Chini kuelekea Juu (BETA), ambayo inapania kukuza sekta ya kilimo.

Richard Oduor, Profesa mashuhuri wa Bayolojia ya Molekuli, Uhandisi wa Kijenetiki, Utafiti wa Dawa, na Sayansi ya Uchunguzi wa Kimaabara, anasisitiza umuhimu wa kuhamasisha na kuwawezesha wakulima kutumia bayoteknolojia za kilimo.

“Kwa nini tulale njaa kama Waafrika? Tunapaswa kutumia mbinu za kilimo zilizopo, zikiwemo mifumo ya bayoteknolojia za kilimo,” anasema Prof Oduor.

Richard Oduor, Profesa mashuhuri wa Bayolojia ya Molekuli, Uhandisi wa Kijenetiki, Utafiti wa Dawa, na Sayansi ya Uchunguzi wa Kimaabara. PICHA|SAMMY WAWERU

Mtaalamu huyu ni Msajili wa Utafiti, Ubunifu, na Ushirikiano katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

Bayoteknolojia ni mfumo unaoshirikisha bunifu za kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoboreka kusaidia kupambana na kero ya kiangazi, wadudu na magonjwa.

Hali kadhalika, unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali.

Kando na manufaa hayo, unapigiwa upatu kushusha gharama ya uzalishaji wa mazao na chakula.

Mfumo huu ukiashiria kuzaa matunda hasa katika nchi zilizoukumbatia, Kenya ikiwemo japo unajikokota, umesaidia kuangazia kero ya njaa na uhaba wa chakula.

Kwa sasa, Kenya inajivunia kilimo cha pamba ya kisasa (Bt cotton), ambayo iliidhinishwa kwa kilimo cha kibiashara 2020 na Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Kibayoteknolojia (NBA).

Pamba ya kisasa, bt cotton, shambani ikiwa imepandwa na mimea mingine. PICHA|SAMMY WAWERU

Kilimo cha bt cotton nchini kilianza 2021, na wakulima wengi wameikumbatia hasa maeneo yanayokuzwa pamba.

Shirika la Utafiti wa Uimarishaji Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), kwa ushirikiano na wadau wengine katika utafiti, limekuwa mstari wa mbele katika kufanya utafiti na majaribio ya mimea kukuzwa kupitia mfumo wa Kibayoteknolojia.

Prof Oduor anasikitika Kenya inaendelea kuwa mateka wa uhaba wa chakula na njaa, ilhali teknolojia za kisasa na bunifu zinaweza kuziba gapu hii.

“Sayansi ipo na ni muhimu sana, na hapo ndipo tunapoleta Bayoteknolojia,” anasema Prof Oduor, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa Masuala ya Bayoteknolojia katika Vyuo Vikuu Kenya.

Mei 2024, NBA iliandaa kongamano lake la 12 la kitaifa Naivasha, jukwaa hilo likiwaleta pamoja wadauhusika kutoka sekta za umma na kibinafsi ambapo walilitumia kutetea teknolojia na bunifu za kisasa kuboresha kilimo.

Mwaka 2022, Rais William Ruto aliondoa marufuku ya miaka kumi iliyowekwa kuzuia ununuzi na uuzaji wa bidhaa za mimea iliyoboreshwa jenetiki (GMO), japo amri yake ilisitishwa kwa muda kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani.

“Mifumo ya Bayoteknolojia katika kilimo inaongeza uzalishaji mazao, kwa sababu kero ya wadudu na magonjwa imepunguzwa kwa kiwango kikubwa,” anasema Dkt Roy Mugiira, Afisa Mkuu Mtendaji NBA.

Dkt Roy Mugiira, Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Kibayoteknolojia (NBA). PICHA|SAMMY WAWERU

NBA ndiyo taasisi ya kiserikali inayojukumika kuidhinisha matumizi ya teknolojia za kisasa na bunifu.

Huku viongozi wa nchi za Afrika wakijitahidi kuangazia usalama wa chakula na baa la njaa, asilimia 55 ya nguvukazi ya bara hili inategemea kilimo kujiendeleza kimaisha.

“Tunapaswa kukumbatia bunifu na teknolojia za kisasa kuboresha kilimo,” anasema Dkt Margaret Karembu, Mkurugenzi Mkuu Acquisition of Agri-biotech Applications (ISAAA) AfriCenter, akisisitiza kuhusu umuhimu wa bayoteknolojia kuzalisha chakula salama.

Dkt Margaret Karembu, Mkurugenzi Mkuu Acquisition of Agri-biotech Applications (ISAAA) AfriCenter. PICHA|SAMMY WAWERU

Dkt Karembu pia ndiye Mwenyekiti wa Open Forum on Agricultural Biotechnology (OFAB) Kenya, jukwaa linalotuza wanahabari waliobobea kuandaa na kusimulia mifumo ya Bayoteknolojia.

Kauli mbiu ya kongamano la NBA 2024 ilikuwa ‘Bayoteknolojia za kisasa na usalama wake kufanikisha Mpango wa Kuinua Ajenda ya Uchumi kutoka Chini kuenda Juu’.

Matumizi ya bayoteknolojia za kisasa katika kilimo yanasifiwa kusaidia kuangazia uhaba wa chakula na njaa.

Mbali na Kenya, nchi zingine za Afrika ambazo zimekumbatia mfumo huo wa kisasa kuendeleza kilimo ni pamoja na Eswatini, Ethiopia, Malawi, Nigeria, Sudan, na Afrika Kusini.

Dkt Roy Mugiira (kushoto) akihamasisha wakulima kuhusu pamba ya kisasa. Kenya ni kati ya nchi zilizokumbatia mfumo wa bayoteknolojia kukuza bt cotton. PICHA|SAMMY WAWERU