Habari Mseto

Magavana wa Pwani wakataa mwaliko wa Rais kujadili muguka


MAGAVANA wa Kaunti sita za Pwani wameukataa mwaliko wa Rais William Ruto kuhudhuria mkutano wa kujadili suala tata la uharamishaji wa muguka.

Magavana hao, wakiwemo Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Andrew Mwadime (Taita Taveta), Fatuma Achani (Kwale), Dhado Godhana (Tana River) na Issa Timmamy (Lamu), walisema mkutano huo ulipangiwa kufanyika Jumanne.

Mnamo Mei, magavana Nassir, Mung’aro na Mwadime walipiga marufuku muguka katika kaunti zao ili kukabili uraibu miongoni mwa vijana, lakini Mahakama ya Embu ikasitisha marufuku hiyo kwa muda.

Kaunti nyingine kama vile Kwale ziliweka masharti makali ya kudhibiti biashara hiyo.

Mnamo Juni 13, magavana hao walipokea mwaliko wa kuhudhuria mkutano na Rais katika Ikulu ya Nairobi kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Mwaliko huo ulitumwa pia kwa Mwenyekiti wa Braza la Magavana Anne Waiguru na wale wa maeneo ambayo miraa na muguka inakuzwa wakiwemo Bi Cicily Mbarire (Embu), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na Kawira Mwangaza (Meru).

“Tunataka kukujulisha kwamba Rais amepanga mkutano mnamo Juni 18, 2024, saa 2.30 alasiri katika Ikulu ya Nairobi kujadili biashara ya miraa/muguka katika kaunti zenu. Tafadhali panga kuhudhuria,” barua kutoka kwa Bw Koskei ilisema.

Hata hivyo, magavana wa Pwani wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Mung’aro wamesema watahitaji muda kukutana na wadau wengine husika na viongozi wa Pwani.

“Tunaomba radhi. Hatutaweza kuhudhuria mkutano huo Jumanne kabla ya kukutana na viongozi wa Pwani, viongozi wa kidini, watetezi wa haki za kibinadamu na wataalamu wa afya ili tuzungumze kwa kauli moja,” alisema Bw Mung’aro.

Kwa wiki kadhaa sasa, viongozi wa Pwani wamekuwa wakitaka kukutana na Rais Ruto ana kwa ana bila kuhusisha viongozi wa sehemu nyingine.

Hii ni baada ya Bw Ruto kukutana na viongozi wa Embu wakiongozwa na Gavana Cecily Mbarire, baada ya magavana wa Pwani kupiga marufuku muguka.

Rais alishutumu marufuku ya magavana

Kwenye mkutano huo, Rais alishutumu marufuku iliyowekwa na magavana wa Pwani dhidi ya biashara hiyo akisema mmea huo ni halali nchini Kenya.

Vile vile, aliahidi Sh500m kwenye Mwaka wa Kifedha wa 2024/25 kuongeza thamani kwa zao hilo.

Hata hivyo, wanasiasa wa Pwani kutoka mirengo ya Kenya Kwanza na wale wa upinzani walimshutumu Rais kwa hatua hiyo wakisema ni ya kibaguzi.

Jumapili, viongozi wa Pwani Bw Mungaro, Bw Godhana, Bw Timamy, Seneta Mohammed Faki (Mombasa) na Danson Mungatana (Tana River), wabunge Owen Baya (Kilifi North), Mishi Mboko (Likoni), Gertrude Mbeyu (Kilifi) Rashid Bedzimba (Kisauni), Danson Mwashako (Wundanyi) na Anthony Mupe (Rabai) walikutana Mombasa na kutangaza hadharani kuwa hawatakubali mwaliko wa Rais.

“Tunamshukuru Rais kwa kutualika kujadili suala la muguka lakini baada ya kujadiliana na viongozi wote tumeamua kuomba radhi. Hatutaweza kukutana naye Jumanne kwa sababu tunataka kukutana na viongozi wote wa Pwani, wataalamu wa afya, washikadau wengine ili tuzungumze kwa kauli moja,” alisema Bw Mung’aro.