Habari Mseto

Mahakama yasitisha mchezo wa paka na panya baina ya Wanjigi na Serikali

Na RICHARD MUNGUTI August 20th, 2024 2 min read

MAHAKAMA kuu imepiga teke na kusambaratisha hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kumshtaki kiongozi wa Chama cha Safina Jimi Wanjigi kumiliki silaha hatari kinyume cha sheria na kusitisha mchezo wa paka na panya kati ya Serikali na mwanasiasa huyo mtajika.

Jaji Bahati Mwamuye alisitisha kufunguliwa mashtaka 11 dhidi ya Wanjigi na DPP.

Kusitishwa kushtakiwa kwa Wanjigi kulizima msururu wa majimbizano makali kati ya mwanasiasa huyo na asasi ya usalama “aliyosema inatumiwa vibaya na maafisa wakuu serikalini kumnyamazisha.”

Jaji Mwamuye alisitisha kushtakiwa kwa Wanjigi aliyekamatwa Agosti 19, 2024 na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kamkunji pamoja na msaidizi wake David Kibe Wakonyo.

Wote wawili wamefunguliwa mashtaka 14. Wanjigi ameshtakiwa kwa makosa 13 peke yake.

Jaji Mwamuye aliombwa atumie mamlaka ya mahakama kuu na kuzima hatua ya DPP kumshtaki Wanjigi ilhali korti ilizima kushtakiwa kwake mnamo Agosti 9, 2024.

“Hii serikali inadharau maagizo ya mahakama na yapasa kuzimwa,” Jaji Mwamuye.

Awali, mawakili wenye tajriba ya juu Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Paul Muite, Dkt John  Khaminwa na Willis Otieno walikuwa wamemuomba hakimu mkuu Susan Shitubi asimame kidete na “kuzuia nchi hii ikirudishwa katika enzi za utawala wa kimla wa hayati Daniel arap Moi”.

“Kesi hii inatazamwa na kufuatwa katika pembe zote. Ni wakati wako usimame na haki na kuzima hatua ya serikali ya kukandamiza haki za Wanjigi. Simama kidete na useme haki kwa Wanjigi,” Kalonzo alieleza hakimu.

Bi Karua naye hakusita kueleza hali ilivyo akisema “ni wazi serikali imeshindwa kutekeleza majukumu yake na sasa imegeukia watu inaowaona kama wapinzani sugu.”

Bi Karua alisema wakati ni sasa haki itendeke na kila Mkenya apate haki yake.

Jaji huyo alielezwa na Dkt Owiso masaibu ya Wanjigi aliyefikishwa mbele ya Bi Shitubi yanatokana na tuhuma kwamba alikuwa anaunga mkono maandamano ya kupinga sera mbaya za serikali ya Rais Ruto yaliyoandaliwa na Gen Z.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwamuye alizima hatua ya kumfungulia mashtaka Wanjigi na Wakonyo.

Jaji Bahati Mwamuye, alisema haki za Wanjigi zimekandamizwa ikitiliwa maanani alikuwa amepewa leseni za kumiliki bunduki na bastola.

Jaji Mwamuye alisema ni jambo la kusikitisha polisi wamekaidi agizo la mahakama kuu la Agosti 9, 2024 kwamba “wasimkamate na kumfungulia mashtaka Wanjigi kuhusiana na umiliki wa silaha.”

Wanjigi, kupitia mawakili wenye tajriba ya juu Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Paul Muite, Dkt John Khaminwa, Jackson Kala, Willis Otieno na Dkt Owiso Owiso walimweleza Jaji Mwamuye kwamba “serikali imekaidi maagizo ya mahakama kuu ya kutomfungulia mashtaka Wanjigi.”

Mawakili hao walimweleza Jaji Mwamuye, mnamo Jumanne (agosti 20) alasiri “iwapo hii mahakama haitazima hatua hii ya kumshtaki Wanjigi itachekelewa na kuonekana haitekelezi majukumu yake kwa mujibu wa sheria.”

Wakili Dkt Owiso Owiso aliyewasilisha ombi hilo la kusitisha kushtakiwa kwa Wanjigi alieleza mahakama wakati umewadia wakati nchi hii itetewe na mahakama.

Kabla ya Jaji Mwamuye kusitisha kesi dhidi ya Wanjigi, hakimu mkuu Bi Susan Shitubi alikuwa amemwachilia kwa dhamana ya Sh10 milioni.

Baada ya kutoka kizuizini, Wanjigi alimtaka Rais Ruto apambane naye kuhusu masuala ya kiuchumi na jinsi ya kuwasaidia vijana waliohitimu vyuo kupata ajira.

Bi Shitubi aliagiza kesi hiyo itajwe Septemba 12, 2024 kwa maagizo zaidi.