Habari Mseto

Makachero wazuia washukiwa wanne wa wizi Kitengela

Na STANLEY NGOTHO July 15th, 2024 1 min read

MAKACHERO katika eneo la Kitengela, Kaunti Ndogo ya Kajiado Mashariki wanaendelea kuwazuilia wanaume wanne wenye umri wa kadri kwa kuwaibia wafanyabiashara vifaa vya kielektroniki.

Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Kitengela David Shabani aliwaongoza wenzake katika oparesheni ambapo wanne hao walinyakwa.

Walipatikana katika chumba kimoja mtaani Kyang’ombe na kunyakwa papo hapo.

Washukiwa hao wanne wanasubiri kufikishwa kortini na wapo kati ya umri wa miaka 22-23.

Simu, vipakatalishi, runinga, kamera, mitungi ya gesi na vifaa na vitu vingine vilipatikana wakati wa oparesheni hiyo.

Kwa mujibu wa polisi, chumba hicho kilichokodishwa, kilikuwa kimejaa vitu na vifaa vilivyoibwa na simu za washukiwa wawili hazikuwa zimezimwa wakati wa kufumaniwa kwao.

Washukiwa hao wanaaminika ni genge maarufu ambalo limekuwa likiwaibia wafanyabiashara na kuwahangaisha wakazi wa Kitengela.

Jana, Jumapili, Julai 14, 2024, watu waliokuwa wameibiwa walifika katika kituo cha polisi cha Kitengela kutambua vitu vyao vilivyokuwa vimeibwa.

Kamanda wa Polisi wa Isinya Patrick Manyasi alisema kupatikana kwa vitu hivyo kulikuwa ni hatua kubwa kwa kuwa wamekuwa wakiwaandama sana wahalifu hao.

“Tunaomba umma uje utambue vitu vyao vilivyoibwa au kupotea. Pia tunalenga kumaliza genge hilo na tuna habari muhimu ambazo zitatusaidia kufikia hilo,” akasema Bw Manyasi.