Akili Mali

Siri ya kuzidisha mapato shambani zaidi ya mboga za kawaida

Na LABAAN SHABAAN September 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA maboma mengi kitongojini Mwarano eneobunge la Kigumo, Kaunti ya Murang’a, makao mengi yana vijishamba vya mboga ya kawaida kama vile sukuma wiki na kabeji.

Lakini shamba moja lina sura tofauti upitapo barabarani katika kiunga kimojawapo cha mji wa Kangari.

Hili ni shamba la mboga aina ya courgette linalomilikiwa na Jane Wambui ambaye aligundua siri ya kufana ni kuwa tofauti na wengine.

Wakati wa kuingia shambani, shamba hili lilikuwa limechanua maua manjano yaliyovutia macho.

Mazao haya ya courgette yamejipachapacha katika safu, zisizokuwa na mwisho, zinazosheneni mimea ya kawaida katika vitongoji mbalimbali vya Mwarano.

“Mimi niligundua wakulima wengi wanalima mboga za kawaida, na sababu hii, bei sokoni huwa si nzuri kwa sababu ya ushindani,” anatanguliza Wambui. “Lakini haina maana kuwa niliacha kukuza kabeji, nyanya, vitunguu na sukuma wiki.”

Mkulima Jane Wambui akishika mazao ya mmea wa courgette shambani mwake, Kigumo, Murang’a. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kulingana na Wambui, courgette ina thamani zaidi ya mboga za kawaida na humvunia mapato makubwa.

“Huwa ninauza mboga zingine lakini courgette iliniongezea mapato kwa njia ambayo sikuamini. Nilishauriwa na wataalamu wa kilimo na tangu hapo sijawahi kuangalia nyuma,” aliongeza.

Kutegema na misimu, bei ya kilo moja ya courgette sokoni huwa kati ya Sh50 na Sh 100.

Shamba lake la nusu ekari humpa angalau kilo 150 ya courgette kila wiki katika msimu wa mimea hiyo kukomaa.

“Lakini mabroka wakati mwingine hutuumiza kwa kununua kilo moja kwa pesa kidogo sana kama vile Sh20,” aliteta Wambui.

Huuzwa sana Nairobi

Madalali wamegundua kuna soko la mboga hizi hasaa jijini Nairobi.

Wao humimika shambani humu aghalabu wakati mimea imekaa shambani kwa angalau miezi miwili.

Huu ndio wakati mwafaka wa mavuno na mkulima huvuna kwa wingi kila wiki mbili kwa kipindi cha hadi miezi sita za ukomavu.

“Wakati mwingine mimi huvuna mara tatu kwa wiki kwa matumizi yangu mwenyewe na kibiashara kwa watu wanaoishi maeneo haya,” alifichua Wambui.

Mkulima huyu hajakuwa na haja ya kutegemea mbinu za kisasa za kidijitali kunadi mazao yake.

Yamkini ni kwa sababu ya sehemu iliko shamba lake; katika barabara inayopitiwa na watu wengi kwa magari na miguu.

“Nadhani mazao haya yanapendwa sana na watu. Nimegundua mabroka wengi huja shambani humu kutaka kununua mboga zangu. Mimi hupendelea wale wanachukua kwa bei nzuri,” alieleza.

Kilimo hai

Mtaalamu wa kilimo Suzianna Wanjiru amekuwa kiungo muhimu katika ustawishaji wa kilimo hiki kwa zaidi ya miaka mitano.

Amefunza wakulima wengi, akiwemo Wambui, umuhimu wa kutumia mbolea ya kiasili na mbinu za kilimo asili.

“Mmea huu aghalabu haushambuliwi na magonjwa na wadudu. Nimekuwa katika safari ya kuhakikisha wakulima wanaepuka zaraa inayotumia kemikali,” anaeleza Wanjiru.

Mazao ya courgettes yaliyokomaa shambani. PICHA | LABAAN SHABAAN