Waliacha kazi za kuajiriwa baada ya kilimo kuwapa donge nono
RACHAEL Wanjiru na Rachael Muthoni ni miongoni mwa wafanyakazi waliotema taaluma zao na kuzamia kilimo mzima mzima Eneobunge la Gatanga Kaunti ya Murang’a.
Awali walianza kilimo wakiwa bado wanaendelea kuchapa kazi walizozisomea chuoni.
Baada ya kugundua mapato ya shambani yako juu zaidi ya mishahara yao, waliamua kupiga teke ajira na kuongeza muda wa kuchuma riziki shambani.
Wanjiru alikuwa mhazili wa shule moja ya sekondari kwa takriban miaka kumi.
Akiwa shuleni, alimwacha mfanyakazi kumtunzia ng’ombe, kuku, mboga na mazao mengine ya shambani.
“Nilipotathmini na kugundua kuwa mshahara wangu kazini ni mdogo sana ukilinganisha na nilichokuwa nikipata shambani, niliamua kuiacha,” anatanguliza.
“Nilikuwa ninafanya kazi kwa muda mrefu kwa sababu nilienda kazini mapema kabla ya saa moja asubuhi na kurudi nyumbani usiku. Nikajiuliza, mbona ninapoteza muda wangu hivi?”
Mfugaji na mkulima
Wanjiru ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, bata mzinga na kuku mbali na kukuza mboga kama vile sukumawiki, kabeji, spinach na vitunguu.
Kadhalika, yeye hukuza malisho ya mifugo wake yakiwemo mahindi na nyasi aina ya napier.
“Ni vigumu sana mimi niende dukani kwa vile ninakuza karibu kila mimea ya chakula… hata majani chai. Siku hizi gharama ya bidhaa ni ghali kwa hivyo nimeamua kujipanga. Dukani mimi hununua vitu vichache sana kama vile sukari.”
Wanjiru anaendelea kusimulia kuwa amependelea kujikuzia miche yake mwenyewe ya mazao anayolima shambani.
Ana vitalu vya vitunguu, spinach, kabeji, dania na karoti.
“Miche yangu mara nyingi hukaa kitaluni kwa angalau majuma matatu hadi mwezi mmoja,” Wanjiru anaambia Akilimali.
“Wateja wangu wengi wanatoka Kaunti ya Murang’a hasaa wanaonunua mboga na maziwa. Kuna baadhi huja hapa kutoka Nairobi kununua maziwa sababu ng’ombe wangu mmoja hutoa maziwa zaidi ya lita ishirini kwa siku,” anaongeza mkulima huyu anayemiliki ng’ombe kumi wa maziwa.
Muthoni pia ana simulizi inayofanana na ya Wanjiru.
Mtaalamu huyu wa teknolojia ya habari na mawasiliano aliamua kutumia muda wake shambani baada ya kushuhudia ufinyu wa mapato katika kazi zake.
“Nilikuwa ninatumia nguvu na wakati mwingi sana kufanya kazi za kukarabati vifaa na mifumo ya elektroniki bila kipato kikubwa. Wakati mwingine hata nilikaa bila kazi,” alieleza Muthoni.
“Niliona watu wengi, ambao hata hawajasoma, wakifanya vizuri shambani. Na kwa sababu kwetu Ndakaini tuna mashamba, nikaamua kujiunga na mama yangu kukuza mboga, mahindi na miparachichi.”
Baada ya kukumbatia kilimo miaka miwili iliyopita, Muthoni alijisajili katika kozi fupifupi kuelewa taaluma ya kilimo asilia.
“Mimi si mkulima tu, nina mtandao wa mamia ya wakulima ambao hunitegemea kupata ujuzi na maarifa ya kilimo,” anaeleza.
Muthoni huzuru mashamba mbalimbali Kaunti ya Muranga ambako kuna wakulima wanaofaidika na maelezo ya mbinu bora za kuboresha kilimo.
“Siku hizi ninasambaza mbolea ya kiasili ambayo haina madhara kwa afya kama zile za kemikali,” aliongeza mkulima huyu ambaye huuza mbolea maalum ya maji kwa wakulima wa Kaunti ya Murang’a.