Wazee wasimulia raha ya kukumbatia kilimo
MURIGI Gichuhi, 65, alikuwa mraibu wa pombe kabla ya kuamua kuchukua mkondo mwingine katika maisha yake.
Anasimulia kuwa alijiondoa kutoka kwa wazee wenzake wenye uraibu wa kunywa pombe na kukimbilia kilimo.
Anakiri kuwa alipoteza wakati mwingi sana na pesa katika vibanda vya wagema mjini Maragua, Kaunti ya Murang’a.
Lakini alipobadilisha desturi hii, maisha yake yamechukua mwelekeo mwingine mzuri uliojaa siha na mapato.
“Niliona hakuna haja ya kukaa maeneo ya burudani na badala yake niwe mtu wa maana kwa maisha yangu, ya familia na ya jamii,” alifunguka mkulima huyu wa maharagwe aina ya French Beans maarufu hapa nchini kama mishiri.
“Shamba langu lilikuwa linakaa bila kufanyiwa kazi wakati huo lakini baada ya mimi kubadilisha mtindo wangu wa maisha, shamba hili limekuwa chanzo changu cha mapato na kunishughulisha ipasavyo. Watu hawakuwa wananithamini nilipokuwa ninapoteza muda wangu mjini na wazee wengine tukibugia pombe bila kujali.”
Katika shamba lake la ekari moja, Gichuhi anakuza mishiri ambayo ana uhakika wa kuiuza sokoni.
Pia ana uhakika wa kupata vibarua wa kazi nyingi za shambani kwa sababu kilimo hiki kinahitaji nguvu-kazi ya kiwango cha juu kidogo.
“Tunashirikiana na wazee wengine wanaofanya kilimo katika eneo hili,” alifichua kuhusu mtindo wa ushirikiano ambao wanasaidiana kukamilisha kazi shambani kufuata utaratibu uliowekwa.
“Kwa mfano, leo tunaweza kulima shamba langu pamoja kisha juma lijalo tuungane kulima shamba la mkulima mwingine.”
Gichuhi ni mmoja wa makumi ya wakulima eneo hili ambao wanajihusisha na kilimo cha mkataba na mashirika yanayosambaza pembejeo.
Wakulima hawa hupigwa jeki hadi asilimia 40 ya mtaji wa kilimo cha mishiri.
Kisha mashirika hununua mazao yanapokomaa kwa bei waliyoelewana na mkulima katika kandarasi.
“Sisi hatuna shida ya kupata mahitaji na maarifa ya kuwezesha kilimo cha maharagwe. Hata ufikiaji wa soko kwetu si changamoto kwa sababu kampuni inayotupiga jeki hununua ili kuuza nje ya nchi,” alieleza Gichuhi.
Mkulima mwingine ambaye aliambia Akilimali kuwa alitengana na uraibu wa kushinda maeneo ya burudani na kuingia shambani ni Joseph Njogu mwenye umri wa miaka 63.
Njogu hukuza mboga aina ya sukuma wiki, spinach na kabeji katika shamba lake la nusu ekari.
“Maisha yangu siku hizi ni ya shambani tu na wala sina muda wa kupoteza katika maeneo ya burudani,” anaeleza Njogu ambaye anakiri maisha yake yameimarika aliposelelea shambani kuchuma riziki.
Soko la mazao yake Njogu yako mjini Maragua na viunga vyake huku wengine wakifika shambani kukusanya mavuno kuuza maeneo ya Thika, Kiambu na jijini Nairobi.