Makala

Aliyekuwa balozi atunukiwa Sh2.5 milioni baada ya kutuhumiwa visivyo kwa utapeli wa shamba

Na SHABAN MAKOKHA February 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Balozi nchini Burundi Ambeyi Ligabo ametuzwa Sh2.5 milioni baada ya kukabiliwa na mashtaka ya uongo ya utapeli katika kesi ya kughushi hati za ardhi.

Kesi hiyo ilianza 2017 wakati Bw Ligabo, ambaye alikuwa Balozi wa Kenya wa Uongozi Bora na Demokrasia katika eneo la Great Lakes Region, alikamatatwa pindi tu aliporejea nchini kutoka Burundi.

Mnamo Agosti 30, 2017 katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege Jomo Kenyatta, makachero walimtia mbaroni.

Bw Ligabo alituhumiwa kwa kuiba ardhi ya mjane, dai ambalo anasema lilimtia kiwewe.

“Nilikamatwa nilipotua, nikatumwa korokoroni kisha kushutumiwa kwa kumpokonya mjane shamba lake,” Bw Ligabo alikumbuka alipojitetea kortini.

Malalamishi dhidi yake yaliwasilishwa na binamu yake Machanja Ligabo ambaye alidai Bw Ambeyi alighushi stakabadhi za kuuza shamba la ekari mbili Kakamega.

Katika nyaraka za mashtaka, kulikuwa na malalamishi manne ya ughushi akituhumiwa alitengeneza hati feki za ardhi Agosti 18, 2008 na kutia saini.

Hata hivyo kesi iligeuka kuwa isiyo na misingi baada ya ithibati za shutuma kukosa.

Wataalamu wa kupiga msasa stakabadhi walithibitisha saini iliyozua mjadala haikuwa ya Bw Ambeyi.

Ilibainika baadaye kuwa mlalamishi, Machanja Ligabo, alikuwa amesafiri nje ya nchi kwa shughuli rasmi wakati wa ‘kutokea kwa tukio la kughushi hati za shamba.’

Licha ya hali hizo za kukanganya kushuhudiwa, kesi hiyo ilijikokota kwa miaka mitatu. Mnamo Septemba 15, 2020, Korti ya Kakamega ilimwondolea Bw Ambaye mashtaka.

Mahakama ilitoa uamuzi ikisema afisa wa uchunguzi alifanya upelelezi usio kamili ama aliwasilisha kesi kortini kwa haraka.

Hakimu Mkuu Mwandamizi Zachariah Nyakundi alisema hakukuwa na ushahidi uliomhusisha na mashtaka ya kughushi.

Baada ya kufutiwa mashtaka, Bw Ambeyi alimshtaki Bw Machanja kwa kumshtaki kwa nia mbaya na kumharibia jina.

Alisema kesi hiyo ilimharibia jina nchini na kimataifa ikizingatiwa amekuwa balozi mwenye tajiriba ya miaka 35.

Korti iliamua kumtunuku Sh1 milioni kuwa jumla fidia kwa kuharibiwa jina na kusumbuliwa kihisia pamoja na Sh1.5 milioni kama malipo maalum kulipia gharama ya kesi.