ANENE: NEMA imesahau kazi yake barabara ya Juja, Nairobi
Na GEOFFREY ANENE
WA KULAUMIWA barabara ya Juja Road kugeuzwa kuwa jaa la taka ni nani? Kwa kiwango kikubwa wafanyabiashara katika barabara hii muhimu wanastahili kuwajibika pakubwa kwa mtindo wao wa kutupa ovyo takataka.
Barabara ya Juja Road, ambayo inatumiwa sana na magari ya mitaa ya Eastleigh, Mathare, Huruma na Kariobangi, ina takataka karibu kila baada ya mita 500 hivi kutoka katika kanisa la Redeemed Gospel mtaani Huruma hadi Shule ya Upili ya wasichana ya Pangani. Sehemu hii ni karibu kilomita saba hivi.
Mitaro katika maeneo haya kando ya barabara ya Juja Road imejaa takataka ya kila aina – karatasi za plastiki, magunia, chupa za plastiki, vyakula vilivyoharibika, na kadhalika.
Maji katika mitaro hii yamesimama, rotuba nzuri ya wadudu kama mbu kuzaana, na magonjwa yanayoletwa na maji machafu.
Kando ya mitaro hii kuna wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula. Mwandishi huyu alipozuru barabara hii alishuhudia mwanabiashara mmoja wa hoteli akimwaga maji machafu yaliyojaa maganda ya mayai bila ya kujali anachangia kuziba kwa mitaro.
Utapata sehemu nyingi tu za biashara zinazopatikana kando ya barabara ni chafu; uchafu ambao unatokana na wafanyabiashara hao wenyewe kutupa takataka ovyo kama alivyofanya mhudumu huyo wa hoteli hiyo ya kibanda.
Inashangaza kwamba watu wanaofanya biashara kando ya barabara hawalipii chochote na ndio wa kwanza kutupa taka kiholela na pia kuleta msongamano wa watu.
“Sisi hatulipi ada kufanyia biashara kando ya barabara wala hatuna leseni kama wale waliojenga maduka kwa kutumia saruji,” alisema mchomaji mmoja wa mahindi kabla ya kuongeza kwamba wao hutozwa faini tu wanapokamatwa na maafisa kutoka Baraza la Jiji na kufikishwa kortini.
Wakokotaji wa mikokoteni pia wanachangia pakubwa katika kuchafua Nairobi. Mwandishi huyu alishuhudia mbururaji wa mkokoteni akifika katika eneo la kanisa la Redeemed Gospel mtaani Huruma na kuanza kupakua mara moja magunia ya takataka aliyokuwa amebeba.
Alisaidiwa na wanaume kadhaa wa familia za kurandaranda kushusha magunia. Familia hiyo kisha ilianza kuchakura katika takataka hizo pengine kutafuta mabaki ya chakula.
Si mara ya kwanza kuona wabururaji wa mikokoteni wakitupa taka kwenye barabara ama hata kando ya barabara.
Wao huonekana wazi wakitupa takataka peupe hata mbele ya polisi wa trafiki katika sehemu hizi ikiwemo katika daraja linalounganisha mitaa ya Kariobangi na Dandora katika eneo la Korogocho.
Kazi kubwa polisi katika barabara ya Komorock Road, ambayo inaunganishwa na Juja Road kwa mzunguko wa Outering Road, inaonekana ni kupokea rushwa kutoka kwa magari ya kubeba abiria na yale ya kibinafsi.
Wafanyabiashara wanaohusika katika kusafirisha taka pia wanachangia katika kuipa Nairobi sura mbaya ya uchafu. Kwa mfano, wakazi wa mtaa wa Kariobangi South Civil Servants wametengewa siku ya takataka kuchukuliwa kupelekwa katika eneo la kutupa taka la Dandora kila siku ya Jumanne.
Si mara moja au mbili, lakini mara nyingi tumeshuhudia takataka zikibebwa siku inayofuata ama hata baada ya siku kadhaa kupita. Kuchelewa kusafirishwa kwa takataka siku iliyotengwa huwapa paka hata mbwa fursa ya kurarua karatasi za kubebea taka wakitafuta chakula na kuifanya kutapakaa.
Malori yanayobeba taka pia yanafaa kumakinika yanapofanya zoezi hili kwa sababu mara nyingi yanapelekwa kwasi na kumwaga uchafu huu barabarani.
Wanunuzi wa bidhaa hawawezi kukwepa lawama wanapotupa taka katika sehemu wanazoishi. Vilevile, si siri kwamba Shirika la Kulinda Mazingira nchini (NEMA) limelala fofofo.
Karatasi za plastiki zinazochangia pakubwa katika kuchafua mazingira zilipigwa marufuku Juni mwaka 2017. Hata hivyo, karatasi hizi ndizo nyingi katika takataka zinazoziba mitaro na kuchafua jiji.
Suluhu ya kuweka mazingira safi ni kila mtu kuchukulia suala hili kwa uzito. Hata hivyo, Kenya itapiga hatua kubwa katika vita dhidi ya takataka kutupwa ovyo wafanyabiashara wakiwa katika mstari wa mbele kuweka maeneo yao ya kazi yanayopatikana karibu na barabara, safi, nayo NEMA iamke kutoka usingizini.