Jamvi La SiasaMakala

Dalili Mudavadi ‘amefunguka macho’

Na JUSTUS OCHIENG April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUMEZWA kwa Chama cha Amani National Congress (ANC) cha Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto, kumeibua wasiwasi wa kisiasa huku baadhi ya wanachama wa zamani wa ANC wakihamia chama kipya.

Baadhi ya washirika wa zamani wa Bw Mudavadi wamejitenga na UDA na sasa wamejiunga na chama kipya cha kisiasa, Umoja Summit Party (USP), ambacho kilifanya NDC yake Alhamisi, Aprili 3, 2025 ili kujipanga kwa mustakabali wa kisiasa.

Japo viongozi wa chama hicho wanajitenga naye, wanasema yeye kama watu wengine anakaribishwa kuwa mwanachama.

Meneja wa zamani wa kampeni wa Bw Mudavadi, Godfrey Kanoti, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa ANC, Barrack Muluka, ni maafisa wa chama hiki kipya cha kisiasa.

Bw Kanoti, ambaye alikuwa msaidizi wa karibu wa Bw Mudavadi, ndiye Kiongozi wa Chama cha USP, huku Bw Muluka akiwa Katibu Mkuu.

“Chama cha ANC kilivunjwa bila kujali wanachama wake. Hawakutushirikisha kujua kama tunataka kujiunga na UDA, bali walifanya uamuzi wao na kukivunja chama, sasa tuende wapi? Tubaki bila chama?” alihoji Bw Kanoti.

Bw Kanoti aliambia Taifa Leo kwamba alijiuzulu kama Mkurugenzi wa Huduma za Utekelezaji wa Serikali (GDS) Januari 9 ili kujipanga kisiasa.

Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa USP na Bw Mudavadi na iwapo chama hicho ni mpango wa kando wake wa kisiasa, Bw Kanoti alisema hawawezi kubaki bila chama kwa kuwa hawakubaliani na UDA.

“Kile tunachofanya ni kuwapa wanachama wetu kote nchini nafasi baada ya kuvunjwa kwa ANC,” alisema.

Alisema USP itajiimarishana kushirikiana na vyama vingine vyenye mtazamo sawa kwa lengo la kuingia mamlakani mwaka 2027.

Katibu Mkuu wa USP, Bw Muluka, alifichua kuwa “mkutano wa Wajumbe wa Kitaifa wa chama chetu huenda ukaamua kutafuta na kuungana na vyama vingine vyenye msimamo kama wetu.”

“Tutaingia katika miungano hiyo mradi tu maslahi yetu hayatawekwa chini ya maslahi mengine yoyote,” alisema Bw Muluka.

Aliongeza: “Tulipojua kuwa ANC ilikuwa inavunjwa, baadhi yetu hatukukubaliana na uamuzi wa kujiunga na UDA, hivyo tulipata marafiki waliokuwa na chama kinachoitwa Umoja Summit Party na tukakubaliana nao kuwa tutashirikiana na kukifufua chama hicho.”

Bw Muluka alisisitiza kuwa ingawa uamuzi wao wa kujiunga na USP hauna uhusiano wowote na Bw Mudavadi, wako tayari kumkaribisha yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho, akiwemo Bw Mudavadi mwenyewe.

“Tunaenda kupanua Kamati Kuu ya Kitaifa, kwa mfano, ili kuwajumuisha watu zaidi,” aliongeza.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa maafisa wa sasa wa USP wataendesha chama kwa muda mfupi tu na baadaye watakikabidhi kwa uongozi wa vijana.

“Tunaenda kukiongoza chama hiki kwa muda mfupi, kukiweka kwenye njia sahihi, kisha kuwaachia vijana waongoze.”

Huku USP ikijiandaa kwa NDC yake, macho yote yatakuwa kwa viongozi wanaounga mkono chama hiki kipya na mkakati wa kisiasa watakaotekeleza.