KITHIMANI, MACHAKOS
MADEREVA, makondakta na abiria walipigwa na butwaa pasta aliyekuwa akiwachapia neno alipokatiza injili ghafla na kutimua mbio.
Ni kawaida kushuhudia katika steji nyingi za magari wahubiri wanachapa neno na kisha kuomba wasafiri wapige jeki kwa kutoa sadaka au fungu.
Pasta huyu hakuwa tofauti. Hakuna aliyejua alikotoka lakini alikumbatiwa kama nabii, na kila siku alikuwa anachapa injili karibu na lango la matatu ili ashawishi wasafiri.
Siku ya tukio akiwa katika pilkapilka zake za kuhubiri alikaribia lango la matatu moja na kuchungulia ndani. Akaona mkono ulionyooshwa kuelekezwa kwake na kudhani anapewa toleo.
Kumbe abiria aliyemnyooshea mkono alikuwa jirani yake nyumbani na pasta huyu alikuwa na deni lake kubwa, ambalo lilifanya mtumishi huyo wa Mungu ahame na kuacha kupokea simu zake.
Pasta alipogundua ni jamaa anayemdai pesa anampungia mkono alikatiza neno mara moja na kutoweka kichochoroni kabla hajanaswa.
Tangu wakati huo mhubiri ameenda maficho na haijulikani iwapo atatokea tena katika steji kuendelea kuchapa injili.