Makala

Familia za polisi zahangaika kufuatia mzozo wa ardhi Westlands

Na FRIDAH OKACHI September 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA za maafisa wa polisi katika kituo cha Loresho, eneo bunge la Westlands, Kaunti ya Nairobi zimefurushwa makwao baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kunyakua ardhi ya kituo hicho.

Mmoja wa familia hizo, ambaye alizungumza na Taifa Leo Dijitali, alisema waliondolewa kwenye ardhi hiyo ambayo ina kituo cha polisi cha Loresho na watu waliovalia mavazi ya polisi wakidai ardhi hiyo inamilikiwa na mtu binafsi.

“Ilikuwa usiku September 16, wakati maafisa kutoka kituo kingine walikuwa na stakabadhi zilizoonyesha kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na mtu binafsi,” alisema mama huyo.

“Walituamrisha kuondoka usiku huo. Maafisa hao pia, waliandamana na watu wengine ambao walitusaidia kufunga mizigo yetu. Tuliachwa kukesha nje wengine wakilazimika kuomba msaada kwa majirani ambao ni wenyeji wa hapa,” aliongeza.

Kulingana na mkazi ambaye ni mwanaharakati kutoka shirika la haki ya kijamii (Loresho Kangemi Paralegal) Bi Betty Humud, polisi hao walihamishwa kutoka kwa shamba la umma lenye ekari sita.

Aliongeza kuwa wakaazi wa eneo hilo walifanya maandamano ya amani kushinikiza mnyakuzi huyo kujitokeza.

“Ukiangalia kwenye ramani ya Mipango ya Kaunti ya Nairobi, shamba hili lenye ekari sita limeorosheshwa kuwa la umma. Polisi na kituo cha Loresho wapo kwenye shamba la umma wala sio la mtu binafsi,” alisema Bi Humud.

Pia, alidokeza kuwa baada ya familia zaidi ya 10 kuhamishwa, walilazimika kuweka malazi na vitu vingine kwenye kontena ili kuomba majirani kuwasaidia sehemu ya kulala.

Sehemu ya mali ya familia za polisi zilizofurushwa. PICHA | FRIDA OKACHI

“Baada ya kuwaondoa maafisa wetu, watu walijenga ua wakidai kuwa walifuata maagizo kutoka kwa mmiliki binafsi. Lakini kufikia leo Septemba 19, 2024, vijana wetu walibomoa ua na kuanza kujengea maafisa wetu upya.”

Mwanaharakati huyo alisema kuwa baadhi ya maafisa kutoka kwenye kituo hicho wanaogopa kuzungumza baada ya kuona mmiliki huyo anafanya kazi na ‘viongozi ambao pia wana usemi.’

Mbunge wa eneo la Westlands Bw Tim Wanyonyi alilaani kitendo hicho akidai kuwa, visa vya wizi wa ardhi vitazidi kushuhudiwa.

Bw Wanyonyi, alimtakata mmiliki huyo kujitokeza na stakabadhi hizo zinazoonyesha kuwa anamiliki shamba hilo.

“Ukuta ambao uliokuwa umejengwa ulionyesha kuwa anamiliki ekari tatu. Mimi na wakaazi wa eneo hili tupo tayari kulinda ardhi hii. Iwapo ni serikali inataka kujenga ina haki ya kuhusisha wakazi kupitia mkutano wa umma,” alieleza Bw Wanyonyi.

Mbunge huyo alikashifu baadhi ya maafisa wa polisi ambao walitumika kuwahamisha maafisa wenzao.

“Kazi ya polisi ni kulinda mwananchi na kulinda mali ya umma. Shamba la umma ni la watu. Hatutaruhusu unyakuzi huu kuendelezwa. Tumeungana pamoja na wakazi kulinda na kurudisha kwa haki kile kinachojulikana ni cha jamii,” alisema Bw Wanyonyi.