FUNGUKA: ‘Nawavizia kuku wageni kazini’
Na PAULINE ONGAJI
SIMO kama anavyojulikana kazini, ni aina ya wale madume ambao mabinti wanapaswa kuepuka kwa vyovote vile.
Unapomtazama, huwezi ukadhani kwamba kaka huyu humudu kuwahadaa mabinti. Yeye ni mwembamba, ana rangi ya maji ya kunde na kusema kweli hana zile sifa ambazo zimejulikana kuwavutia wanawake.
Hana misuli, kifua chake ni chembamba, uso wake ni wa duara dufu na ndevu chache kwenye mashavu. Aidha, sio kwamba amebarikiwa kwa mistari; lakini ajabu ni kwamba hakuna binti huepuka mtego wake mara ya kwanza.
Anafanya kazi kama mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika mojawapo ya kampuni kuu za habari nchini.
Kazini anatambulika kwa tabia yake mbovu ya kutobagua wakati wa kuchagua kiuno cha kubingirisha chumbani. Mabinti kazini sasa wanazijua tabia zake lakini wale wageni hunaswa mtegoni.
“Mimi hunyemelea mabinti kisha kuhakikisha wamenipakulia na natafuna bila haya. Msichana mgeni akiajiriwa, namtambua na kuanza kumwinda. Ili kumnasa, siku za mwanzo mimi huhakikisha kwamba namnunulia lanchi.
Katika kantini yetu kazini, sisi huuziwa chakula kwa Sh100 pekee, na hivyo naweza kumudu kumnunulia lanchi mwezi mzima. Kwa mabinti wapya ambao hawajaanza kupata mshahara mzuri, hilo ni jambo kubwa na ni wakati huo binti huingia mtegoni kisha ghafla bin vu! namnasa na kumtafuna. Nikishamla, namsepa na hata akinipigia simu, hujitia hamnazo.
Ukora wangu siufanyii tu katika idara yetu kwani hata katika vitengo vingine kazini, nimenyemelea ‘kuku’ wageni. Kutokana na kazi yangu, ni rahisi kutambua wageni kwani kazi yetu inahusisha kutembea katika kila idara kushughulikia wafanyakazi kila wanapokumbwa na matatizo ya tarakilishi na mtandao.
Nasikia kwamba tabia yangu inafahamika hadi katika idara ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi, kiasi kwamba mabinti wapya wanapoajiriwa, huonywa dhidi yangu.
Kutokana na sababu hii, nimehamisha shughuli zangu hadi mtandaoni hasa Facebook ambapo huwinda bila wasiwasi. Katika tawasifu ya ukurasa wangu nimeweka aina ya kazi ninayofanya, na hata jina la kampuni yangu.
Kampuni ninayoifanyia kazi ni ya haiba ya juu ambapo mabinti hasa wanaopenda pesa, huvutiwa upesi na hivyo ni rahisi kwao kuingia mtegoni mwangu, kwani wanadhani kwamba napata mshahara mkubwa.
Hicho kimekuwa chambo kubwa cha kuwanasa na hata siwezi kukumbuka idadi ya vipusa ambao wamewahi kuingia mtegoni. Hata kuna kadha ambao wamenianika mtandaoni kwenye kikundi cha Kilimani Mums wakidai kwamba niliwatunga mimba na kuchana mbuga.
Lakini hayo kamwe hayajanizuia kuendelea na shughuli zangu. Aidha, kuna wale wanaonionya mara kadha wakisema kwamba nijichunge kutokana na maradhi ya zinaa ikiwa ni pamoja na Ukimwi. Lakini ikiwa hayajanipata kwa muda huu wote, nini kinachowafanya kudhani kwamba yatanifika sasa? Sina nia kulegeza kamba hivyo sibanduki ng’o!”