Jamvi La Siasa

Gachagua akosa matumaini ya kupona Bungeni, aelekeza nguvu katika Seneti

Na MOSES NYAMORI, SAMUEL OWINO October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kushindwa kutumia mahakama kuzima mchakato wa kumwondoa afisini, wapanga mikakati wa Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa wanaelekeza juhudi zao katika Seneti huku wandani wa karibu wakijaribu kusaka usaidizi kutoka kwa Rais William Ruto.

Japo wabunge wachache waliotia saini hoja ya kumbandua wametangaza kuwa wataipinga Jumanne, wandani wa Gachagua bado wanaamini kuwa hoja hiyo itapita katika Bunge la Kitaifa.

Hata kama wabunge 54 ambao hawakutia saini hoja hiyo watapiga kura ya “La”, Bw Gachagua bado atahitaji wabunge 63 ili kupata angalau wabunge 117 hitaji kumnusuru.
Bw Gachagua sasa anaona Seneti kama ndio asasi mbadala ya kumwokoa baada ya hoja hiyo kupitishwa katika Bunge la Kitaifa katika kikao cha Jumanne.

Wandani wa Gachagua wanaamini kuwa maseneta ni wachache, 67, na wanayo rekodi ya kuzingatia haki na urazini katika maamuzi ambayo wamefiki siku za nyuma.

Wanaamini kuwa wanaweza “kujitetea” barabara kwa idadi hii ya maseneta tofauti na jumla ya wabunge 345 ambao wanatarajiwa kuamua hatima yake kwa kuipigia kura hiyo hiyo Jumanne jioni.

Kulingana na Katiba, hoja hiyo inahitaji kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya wabunge (yaani wabunge 233) katika Bunge la Kitaifa.

Hali ni hiyo hiyo katika Seneti ambapo hoja hiyo iliyodhamini wa Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse inahitali kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya maseneta (yaani maseneta 45).

Kwa hivyo, katika Seneti Bw Gachagua anahitaji kupata uungwaji mkono kutoka angalau maseneta 23 ili kuendelea kushikilia cheo chake.

Wandani wa Gachagua wanaamini kuwa maseneta watashawishiwa na hisia za wananchi wakati wa vikao vya ushirikishaji wa maoni yao, ambapo wengine walipinga hoja hiyo.

Katika Seneti, chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto kina maseneta 31, kikifuatiwa na ODM yake Raila Odinga ikiwa na maseneta 20.

Chama cha Jubilee kinawakilishwa na maseneta watano (5), Wiper (4), UDM (3), Ford Kenya (1), NRA (1) huku chama cha DP kikiwakilishwa na Seneta mmoja.

Vyama vya Jubilee na Wiper vimetangaza kuwa vinamuunga mkono Bw Gachagua.

Taifa Leo imegundua kuwa gavana mmoja amekuwa akifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa kidini akiwaomba wamfikia Rais Ruto kumhimiza aridhiane na Bw Gachagua.

Duru zinasema kuwa gavana huyo ambaye ni mwandani wa Bw Gachagua amekuwa akifanya kila awezalo akilenga kuhakikisha kuwa viongozi hao wawili wanapatana.

Seneta wa Makueni Dan Maanzo pia amethibitisha kuwa juhudi kama hizo zinaendeshwa na wandani wa Bw Gachagua.

“Tunajua kuwa Kanisa linajizatiti kuleta upatanisho kati ya viongozi hawa wawili. Kutokana na hali kwamba wananchi wengi wamepinga hoja hiyo, huenda Rais akawaagiza wabunge kutupilia mbali hoja hiyo,” akaeleza Bw Maanzo.

Jumanne, baada ya wabunge kujadili hoja hiyo kuanzia saa tatu asubuhi, Bw Gachagua atapata muda wa saa mbili kujitetea, kati ya saa kumi na moja jioni na saa moja usiku.

Atajitetea dhidi ya mashtaka 11 yaliyoorodheshwa na Bw Mutuse katika hoja yake. Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula pia alisema kuwa Naibu Rais anaweza kusaidiana na mawakili wake katika utetezi huo au awape mawakili hao kibarua hicho.

Ni baada ya hapo ambapo wabunge wote 345 watapiga kura ama kuunga mkono hoja hiyo au kuipinga.

Idadi jumla ya wabunge ni 349 lakini viti vinne viko wazi.

Viti hivyo ni Banisa iliyobaki wazi kufuati kifo cha Kollow Ali Hassan, Ugunja (iliyosalia wazi kufuatia kuteuliwa kwa Opiyo Wandayi kuwa Waziri), Magarini (ilibaki wazi baada ya ushindi wa Harrison Kombe kufutiliwa na Mahakama) na kiti cha John Mbadi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.