Jamvi La Siasa

Gachagua sasa ataka kikosi chake ‘kutuliza boli’, kiache kumponda Ruto

Na CHARLES WASONGA September 26th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa ameonekana kuanza kulegeza vita vya kisiasa dhidi ya bosi wake Rais William Ruto kwa kuonya wandani wake kukomesha kumshambulia kiongozi wa taifa.

Mnamo Jumanne Septemba 24, Bw Gachagua alianza kwa kumtaka aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Cate Waruguru atulize makombora ambayo amekuwa akimrushia Dkt Ruto na wandani wake (rais).

Mbunge huyo wa zamani, mmoja wa wandani na watetezi sugu wa Bw Gachagua, alikuwa amemtembelea katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

“Nafurahi kutembelewa na dadangu mdogo. Napumzika hapa nyumbani, na sijaenda popote kwani sio Ijumaa. Kesho, nitamwakilishi bosi wangu, Rais William Ruto, katika ufunguzi wa Maonyesha ya Kimataifa ya Kilimo ya Nairobi kwa sababu yuko nje ya nchi,” Bw Gachagua anasema kwenye video inayosambazwa mitandaoni.

Naye Bi Waruguru akajibu: “Ni fahari yangu kukujulia hali na kukuhakishia kuwa Wakenya wamekusalimu na wanakupenda. Na wameniambia nipunguze maneno kidogo.”

“Ndio, sasa punguza hizo, pale ulirusha kali zaidi. Hatupigani na yeyote. Sisi ni wapenda amani na hatuna shida na yeyote. Tutulie na tufanye kazi kwa Wakenya,” Bw Gachagua akamwambia.

Wiki iliyopita, Bi Waruguru aliwashambulia vikali wale aliodai wanapanga njama ya kuwasilisha hoja ya kumtimua afisini Bw Gachagua.

Akiongea katika ibada ya Jumapili katika kanisa la PEFA eneo bunge la Thika Mjini, Mbunge huyo wa zamani alidai Rais Ruto ndiye amewaagiza wabunge hao kuandaa hoja hiyo.

“Rais wetu, ulisaidiwa na Mungu na sisi watu wa Mlima Kenya hadi ukaingi afisi. Tuliadhibiwa vikali kwa kusimama na wewe sasa tunaona unataka kuadhibu Rigathi Gachagua na watu wa Mlima Kenya kwa sababu tumetofautiana na wewe. Hilo halitatendeka,” Bw Waruguru akaonya.

Kwa upande wake Bw Gachagua alisema kuwa yu tayari kuendelea na maisha, endapo hoja hiyo itapitishwa.

“Ni uamuzi wa wabunge. Lakini nilichaguliwa na wananchi na ni wao watathibitisha ikiwa nimefanya kazi nzuri au la. Lakini ikiwa wabunge watashawishiwa au kutishwa ili waniondoe afisini, hiyo ni sawa,” akasema.

Hata hivyo, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen wiki jana, Bw Gachagua alisema hoja kama hiyo itawasilishwa tu bungeni kwa idhini ya Rais Ruto.

“Rais ndiye atapitisha hoja hiyo kabla ya kupelekwa bunge. Ni yeye ndiye atashawishi wabunge kuipitisha. Kwa hivyo, yeye ndiye atakuwa mdhamini wa hoja hiyo,” akamwambia mwanahabari Sam Gituku.