Jamvi La Siasa

Idadi kubwa ya wabunge wa Mt Kenya wamtoroka Gachagua shoka likimkodolea macho

Na JUSTUS OCHIENG’, CHARLES WASONGA September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWELEKEO kuhusu hatima ya Naibu Rais Rigathi Gachagua utajulikana wiki hii hoja ya kumtimua ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni Jumanne.

Haya yanajiri huku idadi kubwa ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya wamemtoroka Naibu Rais wakimsuta kwa kuendeleza siasa za kikabila zinazoweza kuleta migawanyiko nchini.

Hata hivyo, Bw Gachagua amepata uungwaji mkono kutoka mrengo wa Azimio unaongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa, suala hilo linatarajiwa kuwa kwenye ajenda ya mkutano wa Kundi la Wabunge wa Kenya Kwanza utakaongozwa na Rais William Ruto hapo Jumanne (kesho).

Ikiwa mkutano huo utaidhinisha kuwasilishwa kwa hoja hiyo, basi itakuwa wazi kwamba Dkt Ruto anaunga mkono juhudi za kuondolewa afisini kwa Bw Gachagua.

Aidha, anaweza kutumia mkutano huo kuzima kabisa mjadala kuhusu suala hilo na kuhimiza wabunge wa Kenya Kwanza wahubiri umoja nchini.

Kiongozi wa Taifa, ambaye amekuwa ziarani Amerika kuhudhuria Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), alirejea nchini Jumapili jioni.

Hata hivyo, wanasiasa wa mrengo wa Rais Ruto tayari wanadai hoja ya kumtimua Gachagua imepata uungwaji mkono wa wabunge 300.

Kwa upande mwingine, wabunge wandani wa Naibu Rais wanashikilia kuwa jumla ya wabunge 180 wanasimama naye na wameapa kupinga hoja hiyo.

Kulingana na kipengele cha 150 cha Katiba, hoja ya kumtimua Naibu Rais sharti iungwe mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge (yaani wabunge 117 kati ya 349) kabla ya Spika kukubali ijadiliwe.

Baada ya kujadiliwa, hoja hiyo inapasa kupitishwa na angalau thuluthi mbili ya wabunge (wabunge 233) ili ipelekwe katika Seneti ambako pia itahitaji kuungwa mkono na angalau maseneti 47 kati ya 67, ili Gachagua abanduliwe.

Jumapili, mambo yalimwendea mrama zaidi Bw Gachagua baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kutangaza wazi kuwa anaunga mkono mpango wa kumfurusha Naibu Rais.

“Mtu yeyote anayejaribu kuzua vurugu nchini kwa kuhubiri siasa za ukabila na kimaeneo sharti azimwe,” akasema alipohudhuria ibada ya katika Kanisa Katoliki la Wamuyu, Kaunti ya Machakos.

Lakini akiongea Jumamosi katika msururu wa mikutano ya hadhara katika kaunti za Kirinyaga, Embu na Meru, Bw Gachagua alishikilia kuwa alichaguliwa moja kwa moja na wananchi na hivyo wabunge hawana mamlaka ya kumtimua.

Alisema alichaguliwa kwa tiketi moja na Rais Ruto na hivyo ikiwa ataondolewa, kiongozi wa taifa pia anafaa kung’atuliwa.

“Si mimi na rais tulichaguliwa kwa tiketi moja? Kwa hivyo, wale wanataka kunifuta kazi wajue kuwa nikienda………….hata Rais naye …………” akasema aliposimama kwa muda katika kituo cha kibiashara cha Ngurubani, kaunti ya Kirinyaga akiwa njiani kuelekea Embu.

Bw Gachagua aliandamana na wabunge watano pekee akiwemo Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Njeri Maina na Mbunge wa Juja George Koimburi.

Hata hivyo, Bw Musyoka amewaonya wabunge dhidi ya kutia saini hoja ya kumtimua Bw Gachagua akisema mpango huo utatumiwa kuhepa uwajibikaji wa serikalini.

“Na wazi kuwa serikali hii imefeli na sasa imeanza mchezo wa kuelekezana lawama. Kenya Kwanza isihusishe Wakenya katika vita vyao vya kindani.

“Wabunge nao wasikubali kuhongwa Sh100,000 ili waweke sahihi zao katika hoja hiyo, hatutaki kuelekea mkondo huo. Kabla ya kutia sahihi yako jua kuwa hizo ni mbinu ya kukwepa kushughulikia changamoto kadhaa zinazowakabiliwa Wakenya wakati na kufunika sakata kubwa kama vile uuzaji wa uwanja kwa JKIA kwa kampuni ya Adani,” Bw Musyoka akasema akiwa Kitengela, Kajiado.