Jinsi Raila anavyosaidia kudhibiti utawala wa Ruto licha ya dhoruba kali
KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga ameibuka kuwa mwokozi wa serikali ya Rais William Ruto ambayo inakumbwa na hali ya suitafahamu.
Kulipoibuka maandamano yaliyoshinikizwa na vijana dhidi ya Mswada tata wa Fedha wa 2024, Bw Odinga alituliza mawimbi yaliyotikisa meli ya Bw Ruto iliyokuwa imepigwa na dhoruba kali.
Mnamo Julai, Bw Odinga alikabidhi serikali maafisa wake wakuu wa chama cha ODM ambao waliteuliwa katika baraza la mawaziri.
Viongozi hao ni waliokuwa Naibu Kiongozi wa ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa ODM John Mbadi na aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi pamoja na aliyekuwa Mwanachama wa Bodi ya Uchaguzi Beatrice Askul.
Licha ya haya, Waziri Mkuu wa zamani anashikilia kuwa chama cha ODM bado kiko upinzani tofauti na wanavyochukulia wakosoaji wake.
“Hatujaungana na Kenya Kwanza, na iwapo tutaungana, lazima tuwe na mashauriano ya kitaifa kushughulikia masuala tata likiweno suala la Katiba ambalo halijaangaziwa,” Bw Odinga alisema akiwa Mombasa wiki mbili zilizopita akisisitiza alitoa viongozi wake kusaidia serikali kuwa imara.
“Tunahitaji kuwa na mazungumzo ya kitaifa kujadili masuala tuliyoibua na yale ya vijana wakati wa maandamano.”
Tajiriba ya kisiasa ya Bw Odinga imekuwa kimbilio kwa Dkt Ruto hata wakati wa kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Bw Gachagua alituhumiwa kupiga jeki maandamano ya Gen Z dhidi ya serikali mwezi Juni; Bw Odinga alimshika mkono Dkt Ruto katika hoja ya kumtimua bungeni.
Katika mkutano wa pamoja wa Kamati ya Kitaifa (NEC) ya ODM mnamo Julai 2024, Bw Raila aliripotiwa kutilia mkazo shinikizo ya kumtimua Rais Ruto akisema itakuwa ‘hatari’.
“Ruto aende, kisha nini kifanyike? Ruto anaweza kuondoka kisha Gachagua achukue hatamu za uongozi na kutekeleza sera mbaya. Ruto anaweza kusema amechoka, kisha wanajeshi wachukue usukani. Hivyo, nchi itaanza kupitia yaliyokumba Misri wakati wa mapinduzi (Taharir Square). Tukio la Ruto kuondoka haliwezi kuwa mwisho,” alieleza Bw Raila.
“Hatufanyi hivi kumuokoa Ruto. Tunafanya hivi ili kuokoa Kenya. Wanajeshi hawana vitoa machozi. Wana risasi.”
Mchambuzi wa siasa Martin Oloo anasema Rais Ruto anajua hataungwa mkono na eneo la Kati katika uchaguzi wa 2027.
Anaeleza kuwa Rais analenga kuweka kapuni kura za maeneo ya Nyanza na Magharibi akimtumia Bw Odinga katika mpango huu.
“Kwa kumuunga mkono Baba (Bw Odinga) kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), anatarajia kupigiwa kura na Nyanza,” Bw Oloo anasisitiza.
Taifa Leo imebaini kuwa iwapo Bw Odinga atashinda uchaguzi wa AUC, kikosi chake na kile cha Rais kitaingia mkataba kuelekea uchaguzi wa 2027.
Katika mkataba huu, wanatarajiwa kuchora mpango wa kugawana mamlaka ili kushirikisha ODM na chama tawala cha UDA.
Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga anasema hakuna kinachowazuia kufanya kazi na Kiongozi wa Nchi.
Kulingana na Dkt Oginga, jamii ya Waluo itakuwa tayari kulipa deni la kisiasa la 2007 iwapo atatekeleza ahadi zake na kuhusisha jamii yao katika kazi serikalini.
Alitaja kuwa Dkt Ruto alikuwa kiungo muhimu sana 2007 kumfanya Bw Odinga Waziri Mkuu.
“Ninadhani si vibaya kurudisha mkono,” alisema Dkt Oginga.
Naye Rais amedokeza uwezekano wa kuunda muungano na Bw Odinga ambao unaweza kufufua Muungano wa Pentagon wa 2007 kabla ya uchaguzi wa 2027.
Kwa mujibu wa Dkt Ruto, serikali yake jumuishi haijaundwa kwa sababu ya mpango wa kipindi kifupi.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan