Jamvi La Siasa

Jubilee yakoroga hesabu za upinzani kwa kusema itamuunga Raila 2027

Na JUSTUS OCHIENG August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

CHAMA cha Jubilee kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kimeibua mdahalo mkubwa katika siasa kwa kupendekeza kwamba kitamuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2027 japo kwa masharti.

Hatua ya chama hicho imezua tena mvutano ndani ya upinzani na kutia wasiwasi viongozi katika serikali jumuishi ambako Odinga kwa sasa anatekeleza jukumu muhimu kimya kimya.

Makamu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, ambaye ni mwandani wa karibu wa Kenyatta alisema kwamba chama hicho kinaweza kumuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2027, ikiwa tu atakatiza uhusiano wake na serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

Akiongea baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Jubilee jijini Nairobi Jumanne, mkutano wa kwanza tangu kumalizika kwa mfululizo wa kesi za ndani za kuwania uongozi wa chama, Murathe alitangaza kwamba Jubilee bado inamtambua Odinga kama kiongozi wa Azimio la Umoja–One Kenya.

Alisema kuwa chama kinangojea hatua inayofuata ya Odinga kisiasa kabla ya kupanga mkakati wa 2027.

Hata hivyo, maelezo yake yalikinzana na msimamo wa Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni kwamba chama kinaunga mkono Dkt Fred Matiang’i kuwa mgombea urais.

“Tunaendelea kumtambua Raila kama kiongozi wa chama cha Azimio. Kama muungano, tutaamua jinsi ya kuendelea. Lakini naweza kukuambia tuko na Tinga (Raila) hadi tuamue vinginevyo,” Murathe aliambia Taifa Leo, akiongeza kwamba muungano mpya unaweza kuundwa “kumfanya Ruto awe Rais wa muhula mmoja.”

Lakini kauli yake imezua kauli kali ndani ya upinzani.

Kiongozi wa DAP‑K, Eugene Wamalwa, ambaye ni sehemu ya Muungano wa Upinzani unaoongozwa na Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema Odinga anapaswa kwanza kuomba radhi kwa Wakenya kwa kushirikiana na Ruto.

Aliongeza kwamba hata akiachana na Ruto na kurudi upinzani, hatarajiwi kuwa mgombea urais moja kwa moja.

“Tunachotaka kumwambia Raila ni kwanza aombe radhi Wakenya kwa kuwasaliti. Mara atakapofanya hivyo, sisi upinzani bado hatujachagua mgombea urais wetu, hivyo awe tayari kujiunga foleni maana tuna wagombea urais watano,” Wamalwa aliambia Taifa Leo.

“Tuna Eugene Wamalwa (DAP‑K), Fred Matiang’i, Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP) na Rigathi Gachagua (DCP). Tutashindania tiketi hiyo, hivyo Raila akiungana nasi leo, atashindana nasi.”

Wamalwa pia alimkosoa vikali Odinga kuhusu makubaliano ya Machi 2025 na Ruto, akidai ni kinyume cha msimamo wa Azimio na matakwa ya Gen Z.

“Wakenya tayari wameamua kuwa urais wa Ruto utakuwa wa muhula mmoja,” alisema Wamalwa. “Raila atambue hilo haraka na aache ushirika aliotia saini Machi 2025, ni bora kwake na taifa.”

Alidai pia kuwa Odinga aliua Azimio kwa kutoshirikisha vinara wenza kabla ya kusaini MoU na Ruto.

Alisema kwa upinzani kumkaribisha Odinga tena ikiwa ataachana na serikali, lazima aombe radhi Wakenya kisha ajiunge na foleni kushindania tiketi ya urais 2027.

Kauli hizo zinajiri mvutano ukizidi kupamba moto ndani ya ODM kuhusu hatima ya upinzani na mwelekeo ambao Bw Raila Odinga atachukua.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna amekuwa akilaani hadharani muundo wa serikali jumuishi huku baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho wakitofautiana naye.

Naibu Kiongozi wa ODM, Godfrey Osotsi, alionekana kukataa hatua ya Jubilee kuunga mkono Raila kwa masharti, akisema kuwa Bw Odinga hahitaji kuwekewa masharti yoyote.

“ODM inakaribisha msaada kwa kiongozi wetu wa chama, lakini haupaswi kuwa wa masharti,” alisema Bw Osotsi. “Raila amejitolea sana kwa Kenya na amekuwa mzalendo. Si haki kumpa masharti.”

Aliongeza kuwa chama kinaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa 2027, na kitaamua kuhusu miungano wakati ufaao.

Naibu kiongozi wa Democracy for the Citizen’s Party (DCP), Cleophas Malala, alidai kuwa Bw Odinga kwa sasa ni sehemu ya “wale tunaotaka kuwaondoa ifikapo 2027.”

“Kwa maoni yetu, Raila bado anashirikiana na William Ruto. Akiondoka, tutamchukulia kama sehemu ya upinzani. Kwa sasa, bado ni sehemu ya watu tunaotaka waondoke 2027,” alisema Bw Malala.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kila mtu ana mtazamo wake binafsi, na kuongeza kuwa Bw Murathe huenda hakuwa akizungumza kwa niaba ya Jubilee, bali alikuwa akitoa maoni yake binafsi kuhusu Bw Odinga.

Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita, alipuuza pendekezo la Jubilee kumsaidia Odinga, akisema chama hicho kilishindwa kumsaidia hata kilipokuwa na madaraka yote mwaka wa 2022 na sasa hakina nguvu yoyote ya kisiasa.

“Uhuru Kenyatta na Jubilee walishindwa kumfikisha Rao Ikulu walipokuwa na vyombo vyote vya mamlaka. Kufikiria kuwa wanaweza kufanya hivyo sasa wakiwa nje ni upuuzi,” alisema Bw.Nyamita.

Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, alikiri kuwa Jubilee bado imegawanyika, akibainisha kuwa kuna madai tofauti kuhusu mgombea wao wa urais.

Huku Bw Murathe akimuunga mkono Raila, Katibu Mkuu Jeremiah Kioni ametaja jina la Dkt Fred Matiang’i kama mgombea wa Jubilee.

“Kuna kundi la waasi linalomuunga mkono Rais Ruto, na Jubilee halisi inayoongozwa na Uhuru. Ni busara kuacha chama kishughulikie matatizo yake ya ndani kabla ya watu wa nje kutoa maoni,” alisema Bw Wambua.

Tafsiri: BENSON MATHEKA