Jinsi Moi aliangusha na ‘kumfufua’ tena mwanasiasa wa Meru Jackson Itirithia Kalweo
MWAKA 1992 kwenye mkutano wa chama cha KANU katika uwanja wa Mau, Meru, Rais Daniel arap Moi alishtua wengi alipomtangaza Jackson Itirithia Kalweo kuwa miongoni mwa watu wake wa kuaminika kisiasa katika eneo la Meru.
Ilikuwa kauli isiyotarajiwa kutoka kwa Rais, hasa kwa mtu aliyekuwa ametupwa nje ya ulingo wa kisiasa kwa karibu muongo mmoja. Lakini kwa waliomfahamu Kalweo, haikuwa ajabu kabisa.
Alikuwa mzungumzaji mahiri, mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa saikolojia ya mkutano wa kisiasa na kutoa ujumbe uliowasha hisia za umma.
Hakuwa na elimu ya juu, lakini alijua jinsi ya kuibua msisimko kwa maneno yenye mchanganyiko wa utani, ujasiri na hila za kisiasa.
Alikuwa mwanasiasa wa jukwaani, si darasani.
Kalweo alikuwa mshirika wa karibu wa Moi katika miaka ya mwisho ya 1970 hadi mwanzoni mwa 1980.
Baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Nyambene North mwaka 1979, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni na Huduma za Kijamii.
Hata hivyo, jina lake lilipojipata katika orodha ya waliotajwa katika Tume ya Uchunguzi ya Njonjo mwaka 1984, alifutwa kazi na kufukuzwa kutoka KANU.
Tume hiyo ilikuwa silaha ya Moi dhidi ya aliyekuwa Waziri mwenye ushawishi mkubwa, Charles Njonjo, ambaye Rais alimtaja kama msaliti aliyehusika na njama za kumwondoa mamlakani. Kalweo alipata hasara kisiasa kutokana na ukaribu wake wa awali na Njonjo.
Katika uchaguzi mkuu wa 1983, alipoteza kiti chake kwa Joseph Muturia.Baada ya upweke wa kisiasa kwa miaka, Kalweo alirejea KANU baada ya uchaguzi wa 1988. Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la chama katika Igembe, ishara ya kurejesha uaminifu wa kisiasa.
Kufikia mwaka wa 1992, Moi alihitaji sura mpya – au za zamani zilizo tayari kufuata amri – katika maeneo ambako upinzani ulikuwa ukizidi kushika kasi.
Katika eneo la Meru, ambapo DP ya Kibaki na FORD-Asili ya Matiba zilikuwa zimejipenyeza, Kalweo alionekana kama kiongozi aliyefaa kulinda bendera ya KANU.
Na kweli, baada ya Moi kupewa taarifa kuwa Erastus Mbaabu, mshirika wake mwingine, alikuwa akipanga kuhamia DP, alimteua Kalweo rasmi kuongoza kampeni za chama katika Igembe.
Mbaabu alihama KANU kama alivyotarajiwa, na Kalweo alishinda uchaguzi huo kwa urahisi. Kura za urais ziliwaacha wengi vinywa wazi: Moi alipata kura 8,127 dhidi ya 8,870 za Kibaki — tofauti ndogo kwa eneo lililojulikana kuwa ngome ya upinzani.
Kalweo alihusishwa na mafanikio mengi ya maendeleo katika Igembe, hasa kupitia mradi wa Plan International. Miradi kama vile mradi wa maji wa Kawiru, uchimbaji wa visima, na ujenzi wa masoko ilibadili maisha ya wananchi.
Kalweo hakusita kutumia miradi hii kama silaha ya kisiasa: “Nindabuunere nchang’i muthuumu ni keenda bunyua mauta (Nilimuua twiga ili mpate kula mafuta),” alinukuliwa akisema kwa lugha ya Kimeru katika mikutano ya kampeni.
Kwa wakazi wa Igembe, Kalweo alikuwa daraja kati ya serikali kuu na eneo la kaskazini mwa Meru. Moi, kwa upande wake, alitumia ushawishi wa Kalweo kupenya kwenye ngome ya upinzani kwa kuunda wilaya mpya kama Nyambene (Meru North), Meru South (Nithi), na Tharaka.
Katika wadhifa wake wa Waziri wa Masuala ya Ndani, Kalweo alipambana na upinzani mkali bungeni, hususan wakati wa machafuko ya Likoni mwaka 1997 ambapo wapinzani walidai serikali ndiyo ilihusika.
Kalweo, kwa ustadi wake wa kuzunguka maswali, aligeuka kuwa lengo la kejeli za wabunge wa upinzani, hasa alipokuwa akitetea serikali ya Moi.Hata hivyo, jukwaani hakuyumba. Aliendelea kuwa mtetezi mkuu wa Rais. Lakini ushawishi huu haukudumu.
Kufikia mwaka 2002, wimbi la mabadiliko lilivamia Meru North. NARC ya Kibaki, ikiwakilishwa na Kiraitu Murungi, ilimshinda Kalweo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Kalweo alianguka – si tu kama mbunge, bali pia kama nembo ya KANU katika eneo hilo.
Ingawa Kalweo alionekana kutumia wadhifa wake kujinufaisha, kuajiri watu wake, na kuwanyanyasa wapinzani kwa kutumia utawala wa mikoa, wengi wanakubaliana kuwa aliweza kuvuta maendeleo mashinani katika enzi ambayo serikali ya Moi ililaumiwa kwa ubaguzi wa maendeleo.
Kwa mara ya kwanza, Igembe na maeneo ya pembezoni yalipata barabara, maji, shule, na hospitali.
Wengine wanasema, kwa dhati, kwamba: Kalweo alileta serikali karibu na watu wa Meru Kaskazini. Lakini mwisho wa yote, historia ya Kalweo ni mfano wa mwanasiasa wa KANU ambaye alipanda kwa uaminifu wake kwa Rais Moi, akafikia kilele kwa kujua namna ya kupambana jukwaani, na akaporomoka kwa sababu alishindwa kujisawazisha na upepo wa mabadiliko wa mwaka 2002.
Leo, jina lake linakumbukwa si tu kwa ushawishi wake wa kisiasa, bali pia kama kielelezo cha jinsi siasa ya mtegemea-rais ilivyoweza kukuza – na hatimaye kuangamiza – nyota za viongozi wengi katika enzi ya utawala wa chama kimoja.