KINAYA: Ikiwa miaka miwili ya utawala huu inachosha, si saba itaua?
MIMI nimechoka! Wewe hujachoka? Acha kujifanya huelewi ninachomaanisha, unajua vizuri narejelea kuchoshwa na miaka miwili ya utawala wa Zakayo. Na sasa wanasema tuongeze.. tuongeze… tuongeze nini?
Wanasiasa wana mchezo sana. Wanawezaje kupanga kutuongezea miaka miwili katika muhula wa siasa, eti badala ya miaka mitano, uwe na miaka saba?
Ikiwa miwili imetuchosha tayari, wanadhani tutanyamazia saba tu na tuwashukuru kwa kutumia akilia nyingi? Au labda nimechoka peke yangu?
Naamini Mkenya hana subira ya kuongozwa kwa miaka saba na watu asiowapenda, anataka kuwasalimia kwenye debe kila baada ya miaka mitano.
Hata afadhali Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei, angalipendekeza muhula upunguzwe, uwe miaka miwili unusu au mitatu pekee.
Kawaida yetu Wakenya, tunaanza kampeni za uchaguzi ujao mara tu matokeo ya uchaguzi mmoja yakitolewa, hata kabla ya waliochaguliwa kuapishwa. Kusema tusubiri miaka saba ni kutuchokoza bure, na hatutaki ugomvi na mtu.
Hiyo ya kuongeza miaka ni njama ya wanasiasa wetu kwa kuwa wanajua asilimia zaidi ya 80 hawatachaguliwa tena, watakuwa wakiliona Bunge paa, hivyo wanatamani kuendelea kufurahia utamu wa mamlaka.
Au tuseme ni sawa tu, waongeze hiyo miaka iwe saba, lakini iwe na kipengee kinachosema kwamba mbunge, seneta, gavana na rais hafai kutumika kwa kipindi zaidi ya kimoja?
Wazo zuri hilo! Litawaamsha wazembe waliobeba blangeti na kwenda bungeni kulala usingizi wa pono usiojua wakati wa kuamka.
Sheria hiyo ya muhula mmoja-mmoja itawasaidia Wakenya kwa njia nyingi sana ikipitishwa, lakini nitakupa mifano miwili tu: uchu wa mamlaka utaisha kwa kuwa hawatadumu uongozini milele; uongozi utawaniwa na watu walioaminia, si wakora, makahaba na wacheza-kamari.
Katika kuiandika sheria hiyo mpya, inaweza kuwa vyema sana wakiweka kipengee kinachowazuia watu wa familia moja kuwania cheo cha kisiasa wakati mmoja katika muda wa miaka 10.
Hii itatusaidia kuwafungia nje wezi na vizazi vyao vijavyo, tena hawatatumia mali waliyoiba kunata malakani pamoja na watoto wao. Hata sisi ni watoto wa watu, tulizaliwa kama wao, tumejaaliwa vipawa vya uongozi pia.
Nakwambia sehemu hii hasa ikapitishwa inaweza kubadilisha siasa nchini Kenya kwa sababu Zakayo, RAO, MaDVD, Wiper na hata Papa wa Roma wanaweza kwenda nyumbani mara moja!
Ama unafurahia kuona watu hao-hao uliowasoma kwenye vitabu vya chekechea wakiendelea kukukalia mguu wa kausha pamoja na watoto wako?
Zinasikika kama sheria za ulimwengu wa kusadikika, lakini zinaweza kutufaa ajabu. Si lazima sheria zifurahishe kila mtu; mradi zinasaidia idadi kubwa ya Wakenya, basi zinafaa.
Lazima tuwachukulie wanasiasa hatua za kijanja ili wasituangamize. Wawindaji walipojifunza kulenga bila kukosa, ndege nao walijifunza kuruka bila kutua. Ndege wangu tahadhari usifumwe!