Msisimko wa Wantam na Tutam wakumbusha Tanga tanga na kieleweke
Kadri uchaguzi mkuu wa 2027 unavyokaribia, ulingo wa siasa nchini Kenya unazidi kushika joto. Mirengo miwili mikuu ya kisiasa imejitokeza: Timu Wantam (wanaotaka Ruto atawale kwa muhula mmoja) na Timu Tutam (wanaosema atashinda muhula wa pili).
Majina haya, yanayovuma sana mitandaoni na majukwaani, yanaashiria mgawanyiko unaokua ndani ya siasa za kitaifa kwa sababu ya maslahi ya wanasiasa.
Hata hivyo, kwa wale wanaofuatilia historia ya kisiasa nchini, hali hii inarejesha kumbukumbu za timu Tanga Tanga na Kieleweke kabla ya uchaguzi wa 2022.
Tofauti kuu, hata hivyo, ni kwamba wakati wa Tanga Tanga na Kieleweke, kundi la waasi (Tanga Tanga) lilikuwa ndani ya serikali ya Jubilee, likiwa na Naibu Rais William Ruto kama kinara. Leo, hali imegeuka. Kundi la upinzani la Wantam – linajumuisha viongozi waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, lakini sasa wapo nje ya mfumo wa utawala.
Timu Wantam, inayoongozwa kwa sasa na viongozi kama Rigathi Gachagua, Eugene Wamalwa, Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Mukhisa Kituyi, na hata Fred Matiang’i, imeanza kujenga umoja wa upinzani dhidi ya serikali ya Rais Ruto.
“Tumekuwa tukijifunza kutokana na makosa ya zamani. Tunajua jitihada zitafanywa kututenganisha, lakini tunajenga timu yenye nguvu itakayemtuma Ruto nyumbani katika duru ya kwanza,” asema Wamalwa. Kauli hii inaonyesha dhamira ya Wantam kuunda umoja usiotikisika kuelekea 2027.
Kwa upande mwingine, Tutam inajumuisha viongozi wa Kenya Kwanza walioko madarakani, wakiwemo William Ruto, Naibu wake Kithure Kindiki na kiongozi wa wengie katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah. Wao wanapigia debe muhula wa pili wa Rais.
Mwaka wa 2022, waasi waliongozwa na naibu rais na wandani wake – waliokuwa bado na ushawishi serikalini. Mwaka wa 2025 kuelekea 2027, waasi wako nje ya mfumo, jambo linalowaweka katika nafasi ya kuchukua mtazamo mkali wa upinzani wa kweli.
Vivyo hivyo, baadhi ya waliokuwa wapinzani ndio watetezi wa mfumo waliozoea kukosoa wakiwemo wanachama wa ODM wanaotetea Serikali Jumuishi.
“Katika hali hii mpya, wananchi wanapaswa kuwa waangalifu. Mgawanyiko wa kisiasa ni sehemu ya demokrasia, lakini lazima wananchi waangalie zaidi sera kuliko majina ya makundi. Wanapaswa kujiuliza: Je, Wantam wanaleta mabadiliko ya kweli au ni kundi lingine la wanaotaka madaraka? Je, Tutam wanatoa matumaini au ni muendelezo wa matatizo ya sasa?” asema mchanganuzi wa siasa Tom Maosa.
Katika siasa za Kenya, asema, majina hubadilika lakini lengo huwa lile lile la kushinda uchaguzi.
“Mwaka wa 2027 utakuwa mtihani mwingine kwa Wakenya kuonyesha iwapo walijifunza chochote kufuatia uchaguzi wa 2022,” asema.