Jamvi La Siasa

Mtindo wa Uhuru na Ruto uliolemaza jukumu la bunge na kulifanya sehemu ya serikali

Na BENSON MATHEKA February 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la 13 la Kenya limelaumiwa kwa kutekwa na serikali na kuwa zembe zaidi huku Wabunge ambao mamlaka yao ni kuwakilisha, kutunga sheria na kuipiga darubini serikali wakijichukulia kama sehemu ya utawala.

Wataalamu wa siasa na utawala wanasema kwamba kinachoendelea sasa ni mtindo ambao Rais William Ruto alianzisha na mtangulizi wake Uhuru Kenya katika utawala wa Jubilee.

“Walimaliza uhuru wa bunge na kulifanya sehemu ya serikali kuu na hapo ndipo mambo yalianza kwenda yombo. Kwa ufupi, walimaliza nguvu za bunge,” alisema Solomon Kore, mtaalam wa siasa na utawala.

Anasema wawili hao walipuuza Katiba ya 2010, inayoeleza majukumu ya mihimili hiyo miwili ya serikali ambayo rais hana mamlaka makubwa ya kutunga sheria ambayo yametwikwa bunge.

Ibara ya 124 ya Katiba inasema kuwa kila Bunge linaweza kuunda kamati na kutunga Kanuni za Kudumu za kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na vikao vya kamati zake.

“Kamati ni chombo muhimu katika michakato ya kazi ya Mabunge, bila kamati hizi, shughuli za Wabunge zinaweza kukwama. Majukumu ya kamati ni pamoja na kupitia sheria, kupitia na kuidhinisha bajeti na matumizi, kupiga darubini shughuli, sera na mipango ya serikali,” aeleza.

Hata hivyo, kuanza 2020, Serikali Kuu chini ya Rais Uhuru Kenyatta na Ruto akiwa naibu wake walianzisha mtindo wa kusimamia majukumu ya bunge kwa kuteua wenyekiti wa kamati.

Mwaka huo, Rais Uhuru Kenyatta aliwaita wabunge wa Jubilee Ikulu na kuzindua orodha iliyojumuisha kamati 28 za bunge na wanachama wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ambayo ni mwajiri wa wabunge.

Rais Ruto alipoingia madarakani 2022, aliwaita wabunge wote wa Kenya Kwanza na wale wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya walibadilisha nia na kuunga utawala wake.

“Rais Ruto alifuata nyayo za mtangulizi wake na kuwateua wenyeviti wote wa kamati katika Bunge la Kitaifa na katika Seneti. Kulingana na hitaji la katiba la uhuru wa mihimili ya serikali ni kamati zinazochagua wenyeviti na manaibu wao lakini hapa ni rais anayefanya hivyo. Hii inafanya bunge kukosa jukumu lake la kupiga darubini serikali,” aeleza Bw Kore.

Anasema kwa katika hali ya sasa, ni vigumu kuanika matumizi mabaya ya mamlaka kwa kuwa bunge limewekwa mfukoni na serikali na limekuwa likiitetea badala ya kuikosoa.

Kamati za bunge hutathmini mipango na sera za serikali kuona iwapo zinakidhi malengo yaliyokusudiwa ya kisheria, mipango ya maendeleo ya sera, kufanya uchunguzi kuhusu masuala maalum, kukagua na kuidhinisha uteuzi wa wanaoteuliwa na serikali na kutoa jukwaa la ushiriki wa umma katika utekelezaji wa shughuli maalum.

“Lakini katika hali ya sasa, bunge limekuwa la mwosho mmoja huku likiidhinisha sheria na sera zinazobatilishwa na mahakama kwa kuwa kinyume cha sheria,” asema.