Jamvi La Siasa

Nani atazima moto ODM viongozi wakipapurana kuhusu mkataba na UDA

Na CHARLES WASONGA April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HATIMAYE Kiongozi wa ODM Raila Odinga amezungumzia hali ya mkinzano wa kimawazo miongoni mwa viongozi wa chama hicho.

Mgogoro unajiri baada ya ODM kutia saini mkataba wa ushirikiano na chama cha United Democratic Alliance (UDA), chake Rais William Ruto.

Mkataba huo uliotiwa saini na Bw Odinga na Rais Ruto katika ukumbi wa jumba la KICC, Nairobi, mnamo Machi 7, 2025 ulisemekana kulenga kuipa nguvu zaidi serikali jumuishi.

Ni ushirikiano ulioundwa na Dkt Ruto Julai, 2024 pamoja na viongozi wa ODM katika baraza lake la mawaziri.

Kupitia taarifa iliyotumwa kupitia msemaji wake Dennis Onyango Ijumaa Aprili 18, 2025, Bw Odinga amewataka viongozi na wanachama wa ODM kujidhibiti na kuzingatia ungwana wanapojadili masuala yanayojiri serikalini na taifa kwa ujumla.

Waziri huyo mkuu wa zamani alieleza kuwa anafuatiliwa kwa makini uhusiano kati ya ODM na utawala wa Kenya Kwanza na jinsi wadau wengine wanafasiri mkataba huo wa ushirikiano.

Bw Odinga aliahidi kutoa mwelekeo baada ya kukusanya maoni muhimu kuhusu ushirikiano huo, kutoka kwa asasi husika za chama hicho.

Bw Odinga anatambua kwamba majadiliano kama hayo hayaendelei katika ODM pekee kwani yamekuwepo miongoni mwa vyama vikubwa katika mataifa yenye demokrasia iliyokomaa — taarifa kutoka ODM

“Kiongozi wa chama anaonelea kwamba kwa wakati ufaao, asasi husika za chama zitakusanya maoni hayo kinzani na kuandaa msimamo mmoja kuhusu mwelekeo utakaofuatwa. Kwa hivyo, Bw Odinga anawarai wanachama wa ODM na viongozi kuzingatia adabu, ustaarabu, uvumilivu na waheshimiane wanapojadili hali iliyoko sasa nchini na mustakabali wa chama hiki,” ikaongeza.

Bw Odinga pia aliwahakikisha wanachama wa ODM kuwa chama hicho kitadumisha umoja huku kikilenga kushughulikia masuala yenye umuhimu kwa taifa.

Ushauri wa Waziri huyo Mkuu wa zamani umejiri huku ripoti zikichipuza kuwa uhasama umeibuka ndani ya chama hicho baada ya Gavana wa Siaya James Orengo kupinga waziwazi uhusiano kati ya ODM na utawala wa Rais Ruto.

Hali hiyo imepandisha jopo ndani ya chama hicho huku mgawanyiko ukiibuka kati ya viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi na wale wanaipinga.

Bw Orengo, Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ni miongoni mwa wale wanaopinga ushirikiano katika ya ODM na utawala wa Kenya Kwanza.

“Siwezi kusifu serikali kikasuku. Tulipigania Katiba hii inayotoa nafasi kwa watu kuongea bila kudhibitiwa. Nawataka Wakenya wawaambie viongozi wao ukweli. Taifa hili litaangamia ikiwa wanasiasa watageuka wanakwaya wasiohoji maovu yanayotendeka serikalini,” Bw Orengo akasema mnamo Jumamosi Aprili 12, 2025 katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Bw Odinga George Oduor, katika Shule ya Upili ya Ramba, eneo bunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya.

Vitendo vya ukiukaji wa haki

Naye Bw Sifuna, ambaye ni Seneta wa Nairobi akasema: “Kuna watu ambao wanaiharibu sifa ya serikali yake kwa kuendeleza vitendo vya ukiukaji wa haki kama vile kushambuliwa kwa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere kutumia vitoa machozi kule Nakuru. Tafadhali naomba uwadhibiti watu kama hao.”

Kauli za Mabw Orengo na Sifuna ziliwakasirisha viongozi kadhaa wa ODM, wafuasi na wanachama wa muungano wa wasomi kutoka Luo Nyanza, maarufu kama Ramogi Professional Caucus walimtaka Gavana huyo wa Siaya kuomba msamaha kwa Rais Ruto na Bw Odinga la sivyo wadhamini hoja ya kumtimua.

“Gavana Orengo anafaa kufahamu kwamba siasa za kupinga serikali hazijaleta faida yoyote katika kaunti ya Siaya anayoiongoza au eneo la Luo Nyanza kwa ujumla. Isitoshe, Orengo alionyesha utovu wa heshima kwa kumuaibisha Bw Odinga mbele ya kiongozi wa taifa aliyefika kuungana naye kwa mazishi ya mlinzi wake wa miaka mingi George Oduor,” akasema mwenyekiti wa muungano huo, Joshua Nyamori, kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Panafric, Nairobi, Jumatano, Aprili 16, 2025.

‘Atimuliwe ofisini’

“Sasa tunamtaka aombe msamaha kwa Rais, Bw Odinga na jamii ya Waluo kwa ujumla la sivyo hatutakuwa na budi ila kushauri kwamba atimuliwe afisini kwa kosa la kushiriki mienendo isiyokubalika kwa afisa wa hadhi yake,” akaongeza.

Wengine waliomshutumu Bw Orengo ni Naibu Kiongozi wa chama Godfrey Osotsi, Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi miongoni mwa wengine.