Jamvi La Siasa

Njama ya Ruto na Raila kugawanya wapinzani kuelekea uchaguzi 2027

Na JUSTUS OCHIENG March 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa upinzani wanapanga kukutana wiki hii kupanga upya mikakati na kuimarisha ushirikiano wao wakilenga kumuondoa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Haya yanajiri huku kukiwa na madai kuwa Rais Ruto bado anajaribu kuwarai baadhi ya viongozi wa upinzani ili awajumuishe katika serikali yake baada ya kumnasa Bw Raila Odinga wa chama cha ODM.

Kiongozi wa Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), Eugene Wamalwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani, aliambia Taifa Jumapili kwamba Rais amekuwa akifanya juhudi za mara kwa mara kuwashawishi wanachama wao wajiunge naye, lakini wamepanga mikutano mnamo Aprili na Mei ili kuimarisha muungano wao.

“Ndio, tunafahamu juhudi hizi, lakini naweza kukuambia kwamba hatutadanganyika,” Bw Wamalwa alisema. “Kwa mtazamo wetu, siku ambayo Raila na Ruto walitia saini makubaliano yao, ndiyo ilikuwa mwisho wa Azimio. Sasa tuko tayari kupambana nao katika uchaguzi ujao.”

Huku Bw Odinga akisisitiza kuwa yeye si sehemu ya serikali, Mkataba wa Maelewano (MoU) na Rais Ruto unaashiria mwelekeo mpya, na kuzua tetesi kuwa huenda atamuunga mkono Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena 2027.

Kwa muktadha huu, wachambuzi wa siasa wanahoji kuwa viongozi wengine wa upinzani wanapaswa kubaki pamoja na kumuunga mkono mgombeaji mwenye uwezo wa kumenyana na Ruto.

Hata hivyo, Bw Wamalwa ameapa kuwa hawatagawanyika katika azma yao ya kuondoa serikali ya Kenya Kwanza madarakani mwaka wa 2027.

Alisema yeye pamoja na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, na Wakenya wengine wanaotaka mabadiliko, wamekubaliana kuweka kando maslahi ya binafsi ili kuwa na mgombeaji bora wa kupambana na Dkt Ruto kwa manufaa ya taifa.

“Kwa Wakenya wengi, atakayekuwa rais sio muhimu– iwe ni Wamalwa, Kalonzo, Gachagua, Matiang’i au Karua – bali muhimu zaidi ni kuhakikisha William Ruto, anayejulikana kama Zakayo au Kasongo, hatakuwa Rais tena,’ alisema Bw Wamalwa. “Tumemchoka Ruto. Hatuna wasiwasi kuhusu nani atakuwa mgombeaji wa urais au mgombea mwenza. Tunachojua ni kwamba Ruto lazima aondoke.”

Aliongeza kuwa mnamo Aprili na Mei, muungano wao utadhihirika wazi huku Gachagua akitarajiwa kuzindua chama chake.

“Hivyo basi, tutaunda muungano jumuishi wa wananchi ili kuiondoa serikali hii jumuishi. Huku wao wakipanua serikali yao, sisi pia tunapanua upinzani wetu kwa jukumu letu takatifu la kuhakikisha tutampeleka Zakayo nyumbani na kuwaokoa Wakenya kutokana na mateso haya.”

Mchambuzi wa siasa Martin Oloo anasema kuwa siasa za Kenya zimechukua mkondo mpya kufuatia maridhiano ya kisiasa kati ya UDA ya Dkt Ruto na ODM ya Bw Odinga.

“Iwapo upinzani hautaungana na kumchagua mgombeaji mmoja, Ruto na Raila watafadhili wagombeaji wa urais ambao watagawanya kura na kuwapa ushindi wa moja kwa moja,” alisema Bw Oloo.

Bi Karua amesisitiza kuwa kuungana kwao ndio msingi wa harakati zao na dhamira yao ni kumuondoa Rais Ruto mamlakani.